Jumanne, 16 Mei 2023

WAJASIRIAMALI, WAFANYABIASHA WAPIGWA MSASA KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha 

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) katika Mkoa wa Pwani hivi karibuni kilitoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia kwa mwanamke, watoto na makundi maalum kwenye semina iliyoandaliwa na vikundi sita vya wajasiliamali na wafanyabiasha katika Wilaya ya Kibaha. 

Akitoa semina hiyo, Mratibu wa TAWJA, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mhe. Honorina Kambadu alieleza kuwa ukatili wa kijinsia huleta madhara ya afya ya akili, mwili, kimawazo na kifikra na kuathiri uchumi wa Taifa. 

Mhe. Kambadu alitoa elimu kuhusu wosia, haki za watoto, mirathi, talaka na ndoa na kuwasihi wanawake wa vikundi hivyo kuwa makini kutokana na matukio ya ukatili wa kijinsia ambapo wahanga wakuu ni wanawake, watoto na wale wa makundi maalum. 

“Wengi wanafanyiwa ubakaji, ulawiti, rushwa ya ngono, usafirishaji haramu wa binadamu na watoto kutumikishwa katika umri mdogo wa miaka 12 hadi 17,” alisema. 

Mhe. Kambadu aliwahimiza kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na kuzungumza kwa sauti zao zisikike ili kukomesha matukio ya ukatili ambayo husababisha vifo na madhara makubwa. 

Hakimu huyo aliwaeleza wanawake kuwa tofauti kimtazamo baada ya kuelimika na waonyeshe mabadiliko, wawe wa kweli na kuwa mfano chanya kwa jamii. 

“Mama au mwanamke anapaswa kulinda watoto wake na kuwafundisha maadili mema, maana mama anatunza familia kwa upendo  na ndiye mlezi anayekuwa na muda mwingi wa kukaa nyumbani na familia,” alisema. 

Mhe. Kambadu alisema vitendo vya ukatili vimezidi katika jamii kutokana na utandawazi uliopo kuchangia wanawake wengi kuathirika kisaikolojia na kujikuta katika changamoto ya afya ya akili. 

 Kadhalika, Mhe. Kambadu alisisitiza wanawake hao kusikiliza vipindi vya radio, televisheni na kusoma kwenye magazeti ili kujua haki zao za msingi. 

Alitoa wito kwa wanawake wa vikundi hivyo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika maeneo walipo ili kupunguza wimbi hilo na kulitokomeza kabisa. 

Hakimu huyo pia aliwakumbusha kufuatilia kampeni maalum ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iitwayo “Mama Samia Legal Aid Campaign” iliyozinduliwa tarehe 15 Februari, 2023 na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. 

Semina hiyo ililenga kuwaelimisha wanawake kuhusu ukatili ambapo mwanamke ana nafasi kubwa kuupunguza kama akikaa vizuri kwenye nafasi yake nyumbani, ofisini, kwenye biashara na mahali popote anapokuwa.   

Katika semina hiyo, misaada wa baiskeli (wheel chair) ilitolewa kwa baadhi ya watoto mwenye ulemavu ili kuwakomboa katika mazingira magumu waliyonayo.

 

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mhe. Honorina Kambadu akitoa semina kuhusu ukatili wa kijinsia kwa wanawake, watoto na makundi maalum iliyofanyika katika ukumbi ya Destiny Kibaha, Pwani.

Sehemu ya wajasiliamali na wafanyabiasha kutoka Wilaya ya Kibaha wakiwa kwenye semina hiyo.
Wajasiliamali na wafanyabiasha (juu na chini) wakiwa katika makundi ya picha za pamoja.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni