Na Magreth Kinabo- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 16 Mei, 2023 amekutana na ujumbe kutoka Taasisi
ya Kimataifa ya Sheria na Maendeleo
‘International Development Law Organization’ (IDLO) na kuahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa taasisi hiyo katika nyanja mbalimbali za masuala ya kisheria.
Ujumbe huo ulikutana na
Jaji Mkuu katika ofisi yake iliyopo Mahakama ya Rufani Tanzania, Jijini Dar es Salaam,
ambapo alisema Mahakama ya Tanzania imekuwa ikifanya maboresho katika mambo
mbalimbali ya kisheria kuanzia mwaka 2011. Pia katika maboresho hayo imekuwa
ikihusisha wadau wake, ambao ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Taifa
ya Mashitaka na Uhamiaji,
Alisema kuwa Mahakama imekuwa ikishirikiana na IDLO kupitia mkutano ulifanyika Maputo nchini
Msumbiji, ambapo mada ilikuwa ni kuhusu ugaidi. Hivyo katika mazungumzo yao aliishauri
taasisi hiyo kuangalia maeneo ambayo wataweza kushirikiana.
“Tuna maeneo mengi ambayo
tunaweza kushirikiana na mimi nipo tayari kutoa ushirikiano mtakaoutaka,
likiwemo eneo la Kamati ya Kanuni,” alisema Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma aliongeza
kwamba kuna changamoto za ucheleweshaji wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka
katika makosa ya ugaidi, usarifishaji wa binadamu na dawa za kulevya, uharamia
wa majini kwa kuwa makosa hayo yanahitaji ushirikiano wa kimataifa.
Aidha, Jaji Mkuu alifafanua
kuwa hivi sasa kuna makosa ya uhalifu wa kimtandao, hivyo taasisi hiyo inaweza
kuangalia jinsi ya kuweza kushirikiana katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Kiongozi
wa Ujumbe huo, Romualdo Mavedzenge ambaye
ni Meneja IDLO Ukanda wa Afrika alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia maeneo ya ushirikiano hasa
katika kutekeleza mradi wa kuboresha upelelezi, uendeshaji wa mashtaka na
ushughulikiaji wa mashauri ya makosa yanayofanywa kwa kupangwa na kuvuka mipaka
kwa Ukanda Afrika Mashariki. Pia alisema mradi huo unatekelezwa katika nchi 17
za Afrika ili kuwawezesha watu kudai haki zao.
Meneja Mkazi kutoka
Kenya, Tereza Mugazda, alisema katika kutekeleza mradi huo wanaangalia maeneo
matatu ambayo kwa kuyajengea uwezo ambayo ni upelelezi, uendeshaji wa mashtaka
ikiwemo kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama.
IDLO ni taasisi ya
kimataifa isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na kukuza utawala wa sheria na
mwendeleo endelevu yenye makao yake makuu, Roma nchini Italia.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali alipokutana na ujumbe wa Maafisa kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Sheria na Maendeleo yenye makao makuu yake Roma nchini Itali na kwa upande wa Afrika ni Jijini Nairobi Kenya, “International Development Law Organisation” (IDLO) Maafisa hao hawapo pichani leo tarehe 16 Mei, 2023 Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katika) akibadilishana mawazo na sehemu ya ujumbe wa Maafisa kutoka shirika la kimataifa lisilo la kiserikeli linalojihusisha na kukuza utawala wa sheria na maendeleo endelevu (IDLO) mara baada ya kumtemebelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni