Jumatano, 17 Mei 2023

MAHAKAMA SIMIYU YAWAPONGEZA WAFANYAKAZI BORA, WASTAAFU WAAGWA

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mahakama Mkoa wa Simiyu imewapongeza wafanyakazi bora wa mwaka 2022/2023 na kuwaaga wastaafu wanne ambao wamemaliza safari ya kuhumu katika utumishi wa umma mahakamani.

Hafla ya matukio hayo mawili kwa mpigo ilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Simiyu, Bw. Kulwa Dwese.

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita ndiye aliyefungua hafla hiyo ambayo iliambatana na utambulisho kwa watumishi na wageni waalikwa.

Kisha ikafuata risala fupi kutoka kwa mgeni rasmi ambaye aliwapongeza watumishi waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi. Kadhalika, aliwapongeza wastaafu kwa kumaliza utumishi wao vizuri.

“Niwapongeze sana wafanyakazi bora na kuwaomba muendelee kufanya kazi kwa bidii ili mwakani muweze kupata heshima hii tena. Ndugu zangu wastaafu, nawapongeza kwa kumaliza vema kutumikia Serikali yenu, kwani hii inaonyesha ni jinsi gani mlikuwa mkifanya kazi zenu kwa weledi na kumaliza salama bila shida yoyote,” alisema.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa, akizungmza katika hafla hiyo kwa niaba ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, alitoa salamu za pongezi na kuwatakia kila la heri watumishi waliostaafu. Mhe. Kiliwa pia aliwapongeza wafanyakazi bora.

Katika hafla hiyo, Mtendaji wa Mahakama Mkoa aliongoza zoezi la kukata keki kwa kukaribisha mwakilishi wa kila kundi, wakiwemo wastaafu na wafanyakazi bora.

Mgeni Rasmi, Bw. Kulwa Dwese akitoa risala fupi katika hafla ya kuwaaga wastaafu na kuwapongeza wafanyakazi bora.

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akizungumza wakati anafungua hafla hiyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa akitoa salamu.

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu waliohudhuria hafla ya kuwapongeza wafanyakazi bora na kuwaaga wastaafu.

Wastaafu walioagwa wakiwa katika picha ya pamoja.

Wafanyakazi bora wakiwa katika picha ya pamoja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni