Jumatano, 17 Mei 2023

KUMBUKUMBU NYENZO MUHIMU UTENDAJI KAZI WA MAHAKAMA ZITUNZENI; JAJI KIONGOZI

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka watumishi wa Mahakama kuzingatia utunzaji sahihi wa kumbukumbu na nyaraka nyingine muhimu kwakuwa Mhimili huo hauwezi kutekeleza majukumu yake bila kuwa na kumbukumbu zinazohifadhiwa vizuri.

Akizungumza mapema leo tarehe 17 Mei, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakala wa Usalama wa Afya Mahali pa Kazi (OSHA) jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Siyani amesema kuwa, Mahakama ina mifumo mbalimbali ya kutunza nyaraka ikiwemo ile ya masjala ambapo nyaraka halisi zinahifadhiwa.

“Sote tunafahamu tuna njia mbalimbali za utunzaji kumbukumbu lakini pia tuna mifumo ya kielekroniki ya usimamizi wa mashauri, najua mnafahamu kuwa tunao mfumo maalumu wa usimamizi wa mashauri (ACMS) ambao umeboreshwa kutoka kwenye mfumo wa JSDS2 tuliouzoea, ni muhimu kila mmoja kuwa na uelewa wa kuutumia,” amesema Mhe. Siyani.

Jaji Kiongozi amesema wakati huu ambao Mahakama ipo katika safari ya kuelekea matumizi kamili ya TEHAMA katika utoaji huduma, wanalazimika kuendelea kuhifadhi vema kumbukumbu ikiwemo majalada ya mashauri kwenye masjala. 

Aidha, Jaji Kiongozi ameongeza kwamba ana taarifa za kupotea au kutoonekana kwa majalada ya mashauri, ambapo amesema, “tabia hizo zinazofanywa na watumishi wasio waadilifu iwe kwa makusudi au bahati mbaya ni jambo lisilokubalika na ni uzembe wa hali ya juu ambao haupaswi kupewa nafasi na kufumbiwa macho.”  

Mbali na utunzaji kumbukumbu, Jaji Kiongozi amewataka watumishi hao pia kubadili fikra hasi ili kuunga mkono maboresho ya utoaji huduma za Mahakama yanayoendelea kufanyika kwakuwa hayawezi kukamilika na kuleta tija inayostahili bila maboresho ya fikra.

“Sote tunafahamu Mahakama imekwishafanya na inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika utoaji wa huduma, ili mafanikio yetu yawe na tija zaidi, ni lazima wafanyakazi wabadilike kwa kila mmoja wetu kuelekeza fikra zake kwenye kutoa huduma bora,” amesema Jaji Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.

Mhe. Siyani ameongeza kwamba maboresho yanayofanyika hayawezi kukamilika na kuleta tija inayostahili bila kuwa na fikra chanya huku akisisitiza kuwa kila mtumishi ajiulize ni kwa kiasi gani anatoa huduma ambayo kama ikipimwa na watu huru, watakuja na jibu kuwa huduma iliyotolewa ni bora na inaridhisha wateja.

“Ni lazima kila mfanyakazi awajibike kuhakikisha kama tulivyoboresha maeneo mengine, tunaboresha pia eneo hili. Majengo mazuri peke yake bila huduma bora ni bure na huduma bora inatoka kwanza kwa mfanyakazi mmoja mmoja na kisha sote kwa pamoja,” ameeleza Jaji Kiongozi. 

Amebainisha kwamba, tafiti zilizofanyika mwaka 2019, zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango cha kuridhika kwa wananchi kwa asilimia 78 kutoka asilimia 61 kwa mwaka 2015, lakini hicho kisiwe kigezo cha watumishi hao kubweteka. 

Kadhalika, Kiongozi huyo wa Mahakama amewakumbusha pia watumishi hao kuwa na matumizi sahihi ya lugha, uadilifu, muonekano mzuri na mazingira mazuri, kuzingatia muda ili kuwa wepesi wa kutoa huduma kwa wananchi.

“Kuna tatizo la kutoambiana ukweli pale inapotokea kuna ukiukwaji wa maadili, ni lazima tuambiane ukweli. Kuna ugonjwa wa watu kuoneana aibu na hivyo kutowajibishana. Sote tufahamu kuwa, taasisi yoyote ambayo haina uwezo wa kuwajibishana, ni taasisi inayoelekea kuanguka,” amesema Jaji Kiongozi.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Siyani amewataka wajumbe wa kikao hicho kushiriki kikamilifu kutoa hoja zao, changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ili kupata mwarobaini wa hoja hizo.

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote, Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu sana kinachowaunganisha wafanyakazi na uongozi. Baraza la wafanyakazi ni daraja linalotoa fursa kwa watumishi kupitia wawakilishi wao, kujadiliana na uongozi juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine,” amesema Jaji Kiongozi.

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu. Kikao hicho cha siku moja kimefanyika leo tarehe 17 Mei, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakala wa Usalama wa Afya Mahali pa Kazi (OSHA) jijini Dodoma.



Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala kuu wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa kikao cha baraza iliyokuwa ikitolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kulia) pamoja na wajumbe wengine wa meza kuu wakiimba wimbo wa mshikamano daima 'solidarity forever' wakati wa kikao cha aBraza la wafanyakazi wa Mahakama hiyo kilichofanyika leo tarehe 17 Mei, 2023.
Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala kuu, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia), Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Mahakama hiyo, Bw. Leonard Magacha (katikati), Naibu Katibu Mkuu TUGHE, Bw. Rugemarila Rutatina pamoja na wajumbe wengine wa Baraza wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa kikao cha Baraza hilo.
Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Mahakama hiyo, Bw. Leonard Magacha akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.

Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala kuu, Mhe. Sharmillah Sarwatt akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Bw. Rajabu Zuberi akizungumza jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu.
Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi, Bi. Florence Kimaro akipokea cheti cha Mfanyakazi Bora namba moja wa Mahakama Kuu Masjala Kuu.
Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kushoto) akipoketi cheti cha pongezi kwa niaba ya Katibu Mahsusi wake Bi. Scholastica Njiwa ambaye ni Mfanyakazi namba mbili wa Mahakama Kuu Masjala Kuu.
Msaidizi wa Ofisi, Mahakama Kuu Masjala Kuu, Bi.Royaichi Kombe akipokea cheti cha ufanyakazi bora kwa kuwa mshindi wa tatu.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu.
Mhe. Siyani (katikatik) pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka TUGHE (waliosimama)

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni