Na Charles Ngusa - Mahakama Geita.
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Geita na Wilaya zake wameshiriki maadhimisho ya siku ya
wafanyakazi duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa misaada kwa
wodi ya watoto wenye changamoto ya ugojwa wa utapiamlo kwa kutoa sukari, mafuta
ya kula na kupikia, maziwa ya unga pamoja na sabuni ikawa ni mchango wao kwa
jamii wanayoihudumia.
Wakiungana
na taasisi nyingine za kiserikali na binafsi mkoani Geita kuadhimisha kilele
cha siku hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Chama cha Mapinduzi-Kalangalala jana
tarehe mosi Mei, 2023 Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya zake ikiwemo Geita,
Chato, Bukombe, Mbogwe na Nyangh’wale wote walijumuika pamoja.
Akizungumza
kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Muuguzi Kiongozi
katika wodi ya watoto wenye utapiamlo Bi. Generoza Wanna alisema, changamoto hii kwa kiasi kikubwa inatokana
na ukosefu wa elimu kwa wazazi ya namna nzuri ya kotoa lishe bora kwa watoto
jambo ambalo hupelekea watoto walio wengi kupewa chakula cha aina moja tu.
“Nawashukuru
watumishi wa Mahakama kwa kuwakumbuka watoto hao, kwani wadau walio wengi
wamekuwa wakiwakumbuka wahitaji wengine bila kuwakumbuka hawa watoto wenye
utapiamlo na kwamba mahitaji yao yamekuwa na gharama kubwa sana, ndiyo maana
matibabu haya hutolewa bure kwani ni vigumu kwa raia wa kawaida kuyamudu hivyo
anawashukuru kwa upendo wenu mkuu’’, Muuguzi Wanna.
Naye,
mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela akitoa hotuba yake kwa
wafanyakazi, amesisitiza suala la mahusiano kazini (socialization) baina ya
waajiri na wafanyakazi kwani inasaidia kujenga mahusianao mema miongoni mwao.
Mhe.
Shigela akaongeza kuwa, uboreshaji wa mishahara unapaswa kuendana na uzalishaji
katika taasisi husika kama ilivyo kwa serikali ukuaji wa uchumi unaoendana na
uzalishaji mali ndiyo tija ya uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi ikiwemo
mishahara yao.
Kadhalika,
Mkuu wa Mkoa huyo, amewashauri waajiri kujenga utamaduni wa kubaini na
kuzitambau changamoto zinazowakabili wafanyakazi ikiwemo kuwatembelea na
kufahamu maeneo wanayofanyia kazi, vilevile uchumi na bajeti zenu zinaporuhusu muwawezeshe
wafanyakazi wenu motisha kama vile usafiri na makazi bora.
Aidha,
akisoma risala ya wafanyakazi wa Mkoa wa Geita kwa niaba ya vyama vya
wafanyakazi wote, katibu wa TAMICO Mkoa wa Geita Bw. Obedi Mwakapango alisema kuwa, lazima Serikali ijikite katika
kuimarisha fursa za ajira ambazo ni za kujiajiri na kuajiriwa lakini pia ziwe
za staha kwa sekta zote.
Katibu
huyo, aliendelea kwa kuwakumbusha waajiri wazingatie haki na maslahi ya
wafanyakazi wote ikiwemo mishahara bora yenye kuendana na nguvu ambazo
wafanyakazi wanazitoa pamoja na kuzingatia upandishwaji wa madaraja kwa
watumishi wenye sifa. Sambamba na hilo watumishi pia wameiomba serikali
kuangalia upya suala la kikokotoo kwani linaonekana kuwa kandamizi kwa
wafanyakazi.
Kwa
upande wao watumishi wa Mahakama hawakubaki nyuma katika kuzungumzia matumizi
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakamani. Katika maandamano hayo watumishi hao walishika bango lenye ujumbe uliosomeka,MAHAKAMA SASA INAFIKIKA KWA URAHISI KUPITIA TEHAMA”.
ujumbe
huo ulilenga kutoa elimu na kuwakumbusha wadau umuhimu wa matumizi ya TEHAMA
Mahakamani kama njia rahisi ya kupata huduma za kimahakama tofauti na
ilivyokuwa hapo awali ambapo wadau walipaswa kufika Mahakamani ili kuweza
kupata huduma zitolewazo. tofauti na sasa mteja anaweza kupata huduma ya
Kimahakama bila kulazimika kufika Mahakamani mfano, kujua tarehe ya shauri,
kufungua shauri na kusikiliza shauri kwa njia ya mtandao na huduma nyingine
lukuki.
Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Geita wakiwa kwenye matembezi ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi Dunia wakiwa wamebebe Bango lenye ujumbe unaosomeka Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakamani. MAHAKAMA SASA INAFIKIKA KWA URAHISI KUPITIA TEHAMA.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama mkoani Geita wakiwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kuwasilisha ukarimu wao
katika wodi ya watoto wenye utapiamlo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni