Jumanne, 2 Mei 2023

MAHAKAMA MUSOMA YANG’ARA WAFANYAKAZI BORA MEI MOSI

Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, jana iliungana na wafanyakazi duniani kusherekea Siku ya Wafanyakazi inayojulikana kama Mei Mosi.

Maadhimisho hayo katika Mkoa wa Mara yalifanyika katika Viwanja vya Tarafa Sirari wilayani Tarime. Katika maadhimisho hayo, Mahakama Kanda ya Musoma ilikuwa na jumla ya watumishi bora 15 waliochaguliwa.

Wafanyakazi hao bora ambao walizawadiwa vyeti pamoja na fedha taslim ya 500,000/= kila mmoja wametoka Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

Pamoja na maadhimisho hayo, Mahakama Kuu Musoma kupitia kikao chake cha kawaida cha kila Jumatatu asubuhi kilichofanyika leo tarehe 02 Mei 2023, imewapongeza watumishi saba waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora.

Watumishi hao ni Bi. Francisca Swai, Afisa Utumishi, Bw. Thobias Edward, Msaidizi wa Ofisi, Mhe. Donald Sondo, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Bi. Caritas Isilimura, Katibu Mahsusi, Bi. Rose Mukuru, Msaidizi wa Ofisi, Bw. Othman Mlinzi na Bw. Stephen Kibili ambaye ni Dereva. Watumishi hao walizawadiwa fedha taslimu kiasi cha 100,000/= kila mmoja.

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma, wakishiriki katika maandamano ya sherehe za Mei Mosi yaliyofanyika kimkoa Sirari wilayani Tarime.
Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Wilaya Butiama, Bw. Paul Uromi (mwenye fulana ya kijivu) akipokea zawadi ya mfanyakazi bora kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee  aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe ya Mei Mosi Mkoa wa Mara.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya (kulia) akimpongeza Bi. Nossy Merama, Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Mwanzo Sirari kwa kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora.  
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya (aliyevaa kofia na koti rangi ya bluu) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi bora wa Kanda ya Musoma kwa mwaka 2023.  
Mlinzi wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Othman Maulid akipokea zawadi yake baada ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora. Waliosimama pembeni kulia ni watumishi wengine waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora.
Zoezi la kuhesabu kura likiendelea na wanaohesabu kura hizo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Frank Mahimbali (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Marlin Komba (wa kwanza kulia) na Afisa Tawala, Bw. Kandana Lucas (wa kwanza kushoto).

 Watumishi wa Mahakama Kuu Musoma wakifuatilia kwa makini zoezi la kuhesabu kura lililofanyika katika kikao chao cha ndani.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni