Jumanne, 2 Mei 2023

MAHAKAMA YA MKOA WA ARUSHA YAADHIMISHA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI

  . Wafanyakazi wahimizwa kufanya kazi kwa bidii.

Na Seth Kazimoto, Mahakama Arusha.

Wafanyakazi wa Mahakama Mkoa wa Arusha jana tarehe Mosi Mei 2023 walijumuika na Watanzania wengine katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), ambayo yalifanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo katika Jiji la Arusha.

Maadhimisho hayo yalianza kwa kufanya maandamano ya wafanyakazi kuanzia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuelekea uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Katika maandamano hayo wafanyakazi wa taasisi na idara mbalimbali ikiwemo Mahakama walishiriki. Kauli mbiu ya Siku ya Wafanyakazi mwaka 2023 ni “Mishahara Bora na Ajira zenye Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa”.  Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Charles Tiganga alijumuika na wafanyakazi wa Mahakama katika hafla iliyoandaliwa kuadhimisha sherehe ya Mei Mosi. Viongozi wengine wa Mahakama walioshiriki ni Jaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Yahane Massara na Mtendaji wa Mahakama Kuu Arusha, Bw. Leonard Maufi.

Jaji Mfawidhi amewataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili Arusha iendelee kuwa mfano mzuri wa kuwahudumia wananchi.Vilevile, wafanyakazi bora wa Mahakama walitangazwa na kupewa zawadi zao.

Wafanyakazi hao ni pamoja na Msaidizi wa Kumbukumbu Bi. Mary Thomas Kombe kutoka Mahakama ya Wilaya Arusha na Katibu Mahsusi wa Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini Bi. Sikujua Method Maskati ambao walitangazwa na kukabidhiwa zawadi zao na mgeni rasmi. Wengine ni Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Arusha Bi. Kuruthumu Nkundawatu; Msaidizi wa Ofisi Bi. Irene Ndetaramo Mbuya wa Mahakama ya Wilaya Arumeru na Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Mbuguni Bw. Elias Masaki.

Kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Arusha, Bw.Daud Kamwela alisoma risala, na kero mbalimbali zinazowakumba wafanyakazi zilitajwa ikiwa ni pamoja na viwango vya mishahara visivyoendana na gharama halisi za maisha na malimbikizo ya mishahara ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu.

Pia Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Arusha, Mwalimu Lotta  Laizer alizungumzia suala la Kikokotoo na namna lilivyo changamoto kwa wastaafu, ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria hiyo ili kikokotoo kiondolewe kwasababu kinawaumiza wafanyakazi wanaostaafu.

Mgeni rasmi katika hotuba yake amehimiza wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya nchi, na amesisitiza waajiri kutambua na kuwapa tuzo wafanyakazi hodari katika ofisi wanazosimamia. Amekemea tabia ya baadhi ya waajiri kutoa zawadi hewa kwa wafanyakazi hodari na kuongeza kuwa hali hiyo inarudisha nyuma morali ya kufanya kazi kwa wafanyakazi.

“Sitakubali kushiriki kumtangaza mfanyakazi hodari ambaye mwajiri wake hajawasilisha zawadi/tuzo yake hapa meza kuu” alisisitiza mgeni rasmi.

Siku ya Wafanyakazi duniani hufanyika kila ifikapo  tarehe Mosi Mei, ya kila mwaka  duniani kote ambapo wafanyakazi hupata fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa mwajiri ili ziweze kupata ufumbuzi ikiwa ni pamoja na suala la upandaji wa madaraja na ongezeko la mishaha



Mgeni Rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akihutubia wafanyakazi na wananchi waliohudhuria sherehe za Mei Mosi katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhes Joachim Tiganga akiongea na wafanyakazi wa Mahakama Arusha wakati wa maadhimisho Mei Mosi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akiteta jambo na Jaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Yohane Massara (kulia) wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi.



Mtendaji wa Mahakama Kuu Arusha, Bw. Leonard Maufi akimsikiliza kwa umakini Jaji Mfawidhi.

Wafanyakazi bora wa Mahakama mkoa wa Arusha mwaka 2023, kutoka kushoto kwenda kulia; Bi. Irene Ndetaramo, Bw. Elias Masaki, Bi. Sikujua Maskati na Bi. Mary Kombe.

Wafanyakazi wa Mahakama wakifurahia matembezi ya maandamano ya Wafanyakazi siku ya Mei Mosi mkoani Arusha.

Wafanyakazi wa Mahakama walioshiriki maadhimisho ya Mei Mosi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Katibu Mahsusi Bi. Sikujua Maskati, akitunukiwa cheti cha ufanyakazi bora na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela siku ya Mei Mosi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni