·Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi watoa vitabu kuimarisha Maktaba
Na Faustine Kapama na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kuu,
Kazi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose
Mlyambina leo tarehe 3 Mei, 2023 amepokea vitabu vyenye muunganiko wa sheria kutoka
ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa
ajili ya kuimarisha tovuti ya Divisheni hiyo na Maktaba Mtandao ya Mahakama ya
Tanzania.
Tukio la kupokea vitabu hivyo limeshuhudhiwa na Majaji
wengine katika Divisheni hiyo, Mhe. Katarina Mteule, ambaye ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Elimu na Mhe. Biswalo Mganga, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Kuratibu Masuala ya Tovuti, Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Said Ding’ohi, Naibu
Msajili, Mhe. Enock Kassian, Mtendaji, Bw. Samson Mashalla na watumishi wengine.
Vitabu hivyo vimekabidhiwa na Afisa Sheria Mwandamizi
wa WCF, Bw. Deo Victor ikiwa ni siku chache tangu Jaji Mfawidhi alipomtembelea Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma ofisini kwake Kijitonyama Mkoa wa Dar es
Salaam kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana uzoefu.
Akiongea baada ya kukabidhiwa vitabu hivyo, Mhe. Dkt.
Mlyambina amewashukuru WCF kwa mchango wao huo ambao hautatumiwa na
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pekee bali pia Mahakama ya Tanzania kwa ujumla pamoja
na wadau wake.
“Nakala hizi zitaingizwa
kwenye tovuti ya Divisheni yetu na Maktaba Mtandao ya Mahakama ili kuwezesha
watu wengi zaidi, hata katika Mahakama Kuu, Kanda zote nchini ambao
wanashughulikia migogoro ya kazi, kuzitumia kupitia Maktaba Mtandao (e-Library),”
amesema.
Aidha, Jaji Mfawidhi amemshukuru
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na uongozi wote wa
Mahakama kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama (2021 – 2025) hususani nguzo
ya tatu katika kushirikiana na wadau kufanikisha utoaji wa haki.
“Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
ni miongoni mwa wadau wetu, kinachofanyika hapa leo na matokeo ya upatikanaji
wa sheria hizi tulizopewa vina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati
huo, hususani katika nguzo ya Pili ambayo inahimiza upatikanaji wa haki kwa
wakati,” amesema.
Mhe. Dkt. Mlyambina
amesema kuwa WCF kama wadau wameonyesha utayari wa kushirikiana na Mahakama
katika mambo mengi, ikiwemo kudhamini na kutoa
elimu juu ya sheria na shughuli zao zenye uhusiano na migogoro ya kazi,
ununuzi wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya
Maktaba kama vile Komputa na vifaa vingine vya kielectroniki.
Amemshukuru Mkurugenzi
Mtendaji wa WCF na Menejimenti yote kwa majitoleo hayo ambayo yatakuwa na faida
kubwa kwa Mahakama katika kusimamia haki kazi. Jaji Mfawidhi amewaomba kuendelea
kufanya hivyo ili Masjala zote za Mahakama Kuu na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi waweze
kupata nakala za sheria hizo.
Akipokea shukrani hizo, Afisa Sheria Mwandamizi wa WCF alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa uamuzi wake wa kuwatembelea. Amesema ndani ya muda mfupi ujao watatoa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na baadhi ya wadau kuhusu sheria na masuala mbalimbali yanayohusu fidia kwa wafanyakazi.
Bw. Victor amesema hatua hiyo itawawezesha watumishi hao kuwa na wigo mpana wa uelewa wa sheria hizo na utekelezaji wake katika utatuzi wa migogoro ya kikazi inayoletwa mbele yao.
Kadhalika ameahidi kutoa nakala za vitabu hivyo vya kutosha kwa Majaji wote wa Kanda za Mahakama Kuu ya Tanzania nchi nzima ambao wanashughulika na utatuzi wa migogoro ya kazi.
Wakati huo huo, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina
leo tarehe 3 Mei, 2023 ametembelewa ofisini kwake na Wakili Msomi Isaack
Zake na kufanya naye mazungumzo mafupi.
Katika mazungumzo yao, Wakili Zake kutoka Kampuni ya Uwakili ya Zake Advocates ameahidi kutoa vitabu 150
vyenye maudhui ya kisheria vitakavyosaidia Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu kuamua mashauri mbalimbali ya kazi yanayoletwa mbele yao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akisalimiana na Afisa Sheria Mwandamizi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Deo Victor alipowasili ofisini kwake.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na wadau waliohudhuria makabidhiano ya vitabu hivyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni