Jumatatu, 22 Mei 2023

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI LINDI YAPATA MTENDAJI MPYA

Na Hilary Lorry, Mahakama ya Hakimu Mkazi-Lindi

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe. Consolata Singano amewataka watumishi wa Mahakama hiyo kutoa ushirikiano kwa Mtendaji mpya wa ofisi hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuboresha  zaidi huduma za utoaji haki.

Mhe. Singano aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao cha pamoja na watumishi wakati wa kumkaribisha Mtendaji mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Bi.Quip Godfrey Mbeyela. 

“Nakukaribisha kwenye kituo hiki sisi tunaishi kama familia moja tunatakiwa kushirikiana na kusaidiana pale inapotokea changamoto baina yetu, hii itafanya Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi pamoja na Mahakama ya Tanzania kung’ara” alisema Mhe. Singano.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Bi. Quip Godfrey Mbeyela alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kuomba ushirikiano ambapo alisisitiza kwamba, ushirikiano   utarahisisha shughuli za kimahakama ziende kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Lindi, Mhe. Maria Batulaine alisema, wamefurahi kuongezewa nguvu kazi katika kituo hicho hatua ambayo itawapata nguvu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano pamoja na upande wa utawala.

“Tunaomba uruhusu kutusikiliza kwani hapa tuna utii, nidhamu na pia tunarekebishana wenyewe hivyo tunaamini uwepo wako utakuwa chachu wa kudumisha utii na nidhamu iliyopo,” alisema Mhe. Batualine.

Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi ambapo kilihudhuriwa na watumishi wa Mahakama hiyo pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Lindi, Mhe. Maria Batulaine.


Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi  Bi. Quip Mbeyela (aliyesimama) akijitambulisha na kuzungumza machache na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi (hawapo katika picha). Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe.Consolata Singano na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Lindi, Mhe. Maria Batulaine.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe. Consolata Singano (aliyekaa katikati) akifungua kikao na kumkaribisha Mtendaji Mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Mbeyela (kulia), kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Lindi, Mhe. Maria Batulaine.


Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Lindi, Mhe.Maria Batulaine (aliyesimama) akitoa neno la ukaribisho kwa Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Bi. Quip Mbeyela (kulia). Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe. Consolata Singano.

Watumishi wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Lindi wakifuatilia kwa makini kinachojiri katika kikao cha kumkaribisha Mtendaji mpya wa Mahakama hiyo, Bi. Quip Mbeyela (hayupo katika picha).

Afisa Utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Bw. Stephano Morey akiwakaribisha watumishi wa Mahakama hiyo kwenye kikao cha kumkaribisha Mtendaji mpya wa Mahakama hiyo.

(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni