Na Mwinga Mpoli- Mahakama Kuu, Mbeya
Mahakama Mkoa wa Mbeya imezindua programu maalum
itakayowashirikisha watumishi wa kada zote, wakiwemo Majaji kushiriki katika
mazoezi ya viungo ili kujenga afya bora na ushupavu, hatua itakayosaidia
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Programu hiyo ilizinduliwa hivi karibuni ambapo
Majaji, viongozi waamdamizi na watumshi kwa ujumla walishiriki kwenye mazoezi ya
michezo mbalimbali, ikiwemo kukimbia, mpira wa miguu na mpira wa pete.
Akizungumza katika ufunguzi wa mazoezi hayo, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. James Karayemaha aliwapongeza
watumishi kwa kushiriki kwa wingi kwani mazoezi ni afya.
“Kwa hakika, mazoezi ni afya na hii inaongeza ari na
nguvu hata katika utendaji wetu wa kazi, hivyo kutufanya tuweze kuepuka
magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisisitiza Mhe. Karayemaha.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Bw. Teoford
Ndomba alisema atahakikisha vifaa vyote vinavyohitajika vinapatikana kwa wakati
ili kuwapa watumishi nguvu ya mazoezi. Alisema atahakikisha mwalimu wa mazoezi anapatikana.
Kwa upande wao, watumishi wa Mahakama walionyesha kufurahia
programu hiyo ya mazoezi na kuahidi kushiriki bila kukosa kwa kuzingatia ratiba
endelevu itakayotolewa.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni