Na Paul Pascal – Mahakama Kuu-Moshi
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lilian Mongela amekabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake, Mhe. Dkt. Juliana Massabo ambaye amehamishiwa Dodoma kuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika jana tarehe 31/05/2023 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Moshi na kushuhudiwa na Wajumbe wa Menejimenti wa Kanda hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi na za Wilaya za Rombo, Moshi, Siha, Hai, Mwanga na Same.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Dkt. Massabo ameainisha mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake ambayo ni pamoja na kuondoa mlundikano wa mashauri ya muda mrefu, kujenga ushirikiano imara na wadau wa Mahakama katika Kanda hiyo na kuleta upendo na ushirikiano baina ya watumishi.
“Katika kipindi cha miezi tisa niliyoongoza hapa Moshi vilevile tumeweza kufanya jitihada za kutumia TEHAMA kwa asilimia 100,” alisema Mhe.Dkt. Massabo.
Kadhalika, Jaji Massabo ameainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili Kanda ya Moshi ambazo ni pamoja na upungufu wa watumishi, uchakavu wa baadhi ya Mahakama hususani Mahakama za Mwanzo na nyingine.
Kwa upande wake, Jaji Mhe. Dkt. Mongela amemshukuru mtangulizi wake, Mhe. Dkt. Massabo huku akieleza kuwa yote aliyoeleza atayatumia kama funguo za kufungulia milango ya Kanda ya Moshi.
“Mhe. Massabo ninakushukuru kwa hotuba nzuri ambayo kwangu naomba iwe ndio funguo zangu kwa milango ya Kanda ya Moshi. Vilevile niwaombe Viongozi wenzangu katika Kanda hii ule ushirikiano uliokuwepo kwa dada yangu Massabo niombe muuhamishie kwangu ili mambo yaendelee tena kwa kasi zaidi,” alisema Jaji Dkt. Mongela.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lilian Mongela (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji mara baada ya hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi ya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni