Ijumaa, 19 Mei 2023

MSAJILI MKUU AONYESHA MAFANIKIO YA MAHAKAMA KATIKA USIKILIZAJI MASHAURI MWAKA 2022

Na Tiganya Vincent-Mahakama -Dodoma

Mahakama ya Tanzania katika kipindi cha mwaka 2022 imepata mafanikio makubwa eneo la kasi ya umalizaji na uondoshaji wa mashauri kwenye ngazi mbalimbali za Mahakama nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 18 Mei, 2023 na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika Ukumbi wa Jengo la PSSF jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya hali mashauri mwaka 2022.

Alisema hali hiyo inatokana na wastani wa muda unaotumika tangu kufunguliwa hadi kumalizika kwa shauri.

Mhe.Chuma alisema hadi Disemaba mwaka 2021 mashauri 64,001 yalibaki na mwaka 2022 mashauri 243,597 yalifunguliwa wakati mwaka huo ni mashauri 257,299 yalisikilizwa na kubaki 50,300.

Alisema hadi Disemba mwaka 2022 mlundikano wa mashauri yaliyokuwa 2,962, ikiwa ni sawa na asilimia 6.

Mhe.Chuma aliongeza kuwa kati ya Januari hadi Aprili mwaka 2023 mashauri yaliyofunguliwa ni 85,560 na mashauri 82,831 yalisikilizwa, ikiwa ni sawa na asilimia 97.

Msajili Mkuu huyo wa Mahakama alisema mlundikano wa mashauri umepungua kutoa asilimia 11 mwaka 2021 na kufikia asilimia 6 mwaka 2022 na mwaka 2023 kufikia asilimia 3.

Mhe. Chuma alisema kuwa kiwango cha umalizaji wa mashauri umeongezeka kutoka asilimia 99 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 106 mwaka 2022.

Alisema mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha uondoshaji wa mashauri kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi kufikia 84 mwaka 2022.

Aidha, Mhe Chuma alisema wastani wa muda wa tangu kufunguliwa hadi kumalizika kwa shauri umepungua kutoka siku 119 mwaka 2021 hadi kufikia siku 95 mwaka 2022.

 Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akitoa taarifa ya juu ya hali ya mashauri mwaka 2022 jana tarehe 18 katika Mkutano wa Baraza la Wanyakazi wa Mahakama ulifanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa PSSF jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania (juu na chini) wakifuatilia taarifa ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (hayupo katika picha) wakati wa mkutano wa siku mbili ulioanza jana tarehe 18 Mei 2023.

Picha na Tiganya Vincent- Mahakama -Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni