Stephen Kapiga -Mahakama Mwanza.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wafanyao kazi katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), jijini Mwanza wameaswa kuendelea kudumisha upendo na ushikamano baina yao ili kuweza kufanikiwa kutimiza majukumu yao katika utumishi wa umma yatakayowawezesha kuwa na matokeo chanya katika kazi zao za kila siku.
Rai hiyo imetolewa tarehe 27 Juni, 2023 katika hafla fupi ya kumuaga Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Mwanabaraka Mnyukwa aliyehamia katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) kilichopo Temeke, jijini Dar es Salaam ambapo amepangiwa kuwa Jaji Mfawidhi.
“Nawasihi kuwa na upendo na umoja baina yenu katika majukumu yenu ya kila siku.Upendo mlionionesha tangu niwe nanyi hapa Mwanza nawaomba muendelee kuuonesha kwa wengine waliopo na watakaokuja pia.Kufanya hivyo itasaidia kurahisisha majukumu yenu ya kazi kila siku.Nakumbuka niliokuwa nafanyanao kazi katika chumba changu hakuna aliyekuwa akilalamika kutokana na majukumu tuliyokuwanayo bali tulisaidiana kwa sababu ya upendo uliokuwepo” amesema Mhe Jaji Mwanabaraka.
Aidha kwa upande wake Jaji Mfawadhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt Ntemi Kelekamjenga amemshukuru Mhe. Jaji Mwanabaraka kwa kipindi chote walichofanya kazi pamoja katika Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Mwanza na kusema kuwa kuna mengi wamejifunza kutoka kwake na kumtakia kila lililo kheri kwenye majukumu yake mapya katika Kituo hicho.
“Mhe Jaji Mwanabaraka Mnyukwa nimefanya nae kazi kwa kipindi kirefu tangu tukiwa wote katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, natambua uchapakazi wako, Na tangu nimefika Mwanza nimefanya kazi na wewe kwa takribani miezi sita, hivvo kuna mengi tumeweza kujifunza kutoka kwako na tunakutakia baraka tele katika majukumu yako mapya na Mungu atakusaidia utaweza kuyatekeleza yote” amesema Mhe .Jaji Dkt. Kelekamajenga.
Hafla hiyo fupi iliyoondaliwa na watumishi hao imekuwa ya kufana kwani watumishi wote walionekana kukuguswa na tukio hilo na kuweza kumpatia zawadi mbalimbali Mhe Jaji Mwanabaraka kama kumbukumbu ya kuwa waliwahi kufanya kazi pamoja katika Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mwanza.
“Mhe Jaji tumekupatia kidogo hicho kama zawadi tukiwa kama watumishi wa jengo hili la IJC Mwanza kwani tunakumbuka jinsi ulivokuwa ukijali muda na hata matukio mbalimbali yaliyokuwa yakitokea hapa katika jengo letu,hivvo kwa zawadi hizo tuonamba iwe kama kumbukumbu kwako kwa yale yote tuliyoweza kushirikiana ukiwa hapa IJC Mwanza.” Amesema Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Bw. Tutubi Magazini.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akikata keki maalumu iliyoandaliwa kwa ajili kumuaga katika Sheree Tupi iliyofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC). Mwanza.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni