Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina amewahimiza Watanzania kujengea tabia na bidii
ya kusoma, kufanya tafiti na kuandika vitabu, hasa kwenye taaluma ambazo wanazifanyia
kazi, ili kuwa na uelewa mpana katika mambo mbalimbali, ikiwemo sera na sheria.
Mhe. Dkt. Mlyambina ametoa rai hiyo leo tarehe 28
Juni, 2023 kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Divisheni hiyo wakati wa kupokea
kutoka kwa Wakili wa Kujitegemea, Msomi Ally Kileo nakala 10 za Kitabu kinachoitwa
“Comprehensive Issues of Employment and Labour Law” ambacho kimesheheni utafiti
kuhusu masuala na sheria za kazi.
“Ni jambo ambalo tunapaswa kulihimiza kwa kila Mtanzania,
kila taaluma iwe na dhamira ya dhati ya kufanya tafiti, kusoma, lakini pia
kuandika. Ukitaka kuelewa mambo mengi kwenye taaluma yako huwezi kuyapata
sokoni au kwenye maeneo mengine ambayo yapo nje ya kujisomea. Tuwe na bidii ya
kusoma, kufanya utafiti na kuandika yale ambayo hasa tunayafanyia kazi,”
amesema.
Mhe. Dkt. Mlyambina amesema kuwa Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ambayo ndiyo mwongozo mkuu wa haki kazi
inabainisha madhumuni makuu saba, ikiwemo kukuza maendeleo ya kiuchumi kupitia
ufanisi katika uchumi, uzalishaji na haki ya jamii. Amesema madhumuni hayo ndiyo
msingi wa mikakati mbalimbali ya Mahakama inayozingatiwa katika utoaji haki.
Jaji Mfawidhi amesema mikakati endelevu ya Mahakama ni
kutoa haki kwa wakati ili kuwafanya wadaawa na wadau wajikite zaidi katika
uzalishaji, hatua ambayo ni utekelezaji wa nguzo ya pili ya Mahakama inayohimiza
upatikanaji wa haki kwa wakati.
Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi, ili haki iweze kupatikana
kwa wakati yapo mambo mengi ambayo yanachangia, ikiwemo kuwa na uelewa mpana
juu ya sera na sheria mbalimbali na ili mtu kuwa na uelewa mpana, hawezi kukwepa
kusoma vitabu, majarida mbalimbali na machapisho ya kila namna.
“Bahati mbaya sana sisi Watanzania siyo tu wavivu wa
kusoma, lakini pia wavivu zaidi wa kuandika. Tunapoona wenzetu wametoa muda wao
wakafanya utafiti wa kina, wakaleta mawazo yao na kuyaweka pamoja kwenye makala
mbalimbali, ikiwemo vitabu ni jambo ambalo tunapaswa kulipongeza kwa kila namna,”
amesema.
Jaji Mfawidhi amempongeza Wakili Msomi Kileo kwa
uzalendo aliouonyesha na kuweza kuandika kitabu chenye kurasa zisizopungua 1000,
tena chenye utafiti wa kina kuhusu sheria za kazi, jambo ambalo halikuwa rahisi
kwa vile lilihitaji muda mwingi, rasilimali kubwa na kujitolea.
Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote,
hasa Mawakili na wengine waliopo kwenye Vyuo Vikuu kutenga muda wa kuandika
vitabu vya Kitanzania ambavyo vinaelezea mazingira yanayowazunguka, badala ya
kuwa tegemezi ya vitabu vya nje, ambayo pengine haviendani na mazingira yaliyopo.
“Tukipata fursa ya kuandika sisi wenyewe vitakuwa ni
vitabu ambavyo vitatusaidia sana katika kukuza uchumi wetu kwa ajili ya
mazingira ya sasa lakini pia kwa ajili ya vizazi vijavyo. Tukitegemea vitabu na
makala za nje havitasaidia katika kukuza uchumi wetu wa ndani,” amesisitiza
Mhe. Dkt. Mlyambina.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitabu hivyo, Msomi
Kileo alimshukuru Jaji Mfawidhi na Mahakama kwa ujumla ya kupewa fursa hiyo. Alieleza
dhima kuu ya kitabu chake ambayo ni uchambuzi wa Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini, lengo likiwa kuelimisha waajiri na waajiriwa kuhusu haki na stahiki za
pande zote mbili ili kupata ufahamu na kuepuka migogoro ya kazi, hivyo kuleta
tija katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.
Amesema, ajira na mahusiano kazini yamekuwa na
historia ndefu Tanzania, lakini mabadiliko ya sheria yameweza kukuza sheria na
tafsiri za sheria hasa kupitia Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi. “Maamuzi mbalimbali
ya Mahakama yameendelea kuleta tafsiri mbalimbali za sheria. Kitabu hiki
kimechambua tafsiri hizo kwa kina na kutoa mapendekezo ya mabadiliko katika
maeneo mbalimbali kulingana na mazingira ya nchi yetu,” Wakili huyo amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuwashauri Mawakili na
wawakilishi wa wafanyakazi kutoka vyama vya wafanyakazi kuendelea kushauriana
na waajiri na waajiriwa ili kupata tafsiri sahihi ya sheria. Msomi Kileo amebaini
pia katika utafiti wake kuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, kwa namna
moja au nyingine, inaonekana kuwapendelea waajiriwa kuliko mwajiri. Hivyo amependekeza
mambo kadhaa katika kitabu chake katika uwepo wa haki sawa katika jamii.
Kwa upande wake, Wakili Msomi Matojo Kusata
aliyeambatana na Msomi Kileo kwenye tukio hilo ameonyesha kufurahishwa na
utaratibu huo na kuahidi katika siku chache zijazo kutoa nakala laini ya vitabu
kadhaa vitakavyosaidia Mahakama katika utatuzi wa migogoro ya kazi.
Wakili huyo amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria inayoitwa
the Tanzania Library Services Act, Cap
102, 1975 na the Publications (Compulsory
Deposit) Order, 1964, ni takwa la kisheria kwa kila mchapishaji na
mwandishi kupeleka katika Maktaba ya Taifa angalau nakala mbili ya kila chapisho
ndani ya mwezi mmoja tangu siku ya uchapishaji huo. Hivyo, ameshauri utaratibu
huo ufanyike pia kwenye Mahakama na taasisi zingine muhimu, hatua ambayo itasaidia
kukuza uelewa katika maeneo mbalimbali.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu,
Mhe. Cassian Matembele na Kaimu Mtendaji wa Divisheni hiyo, Bw. Jumanne Muna, watumishi wengine wa Mahakama hiyo na Mawakili wawili walioambatana na Msomi Kileo.
Viongozi wa Mahakama waliohudhuria hafla hiyo. Kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Cassian Matembele na Kaimu Mtendaji wa Divisheni hiyo, Bw. Jumanne Muna.
Wakili Msomi Ally Kileo (kushoto) akiwa na Mawakili wengine wawili ofisini kwa Jaji Mfawidhi kabla ya kukabidhi vitabu hivyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni