Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, imeazimia kumaliza mashauri ya muda mrefu kwa kushirikiana na wadau wa Haki Jinai Mkoani Manyara.
Maazimio hayo yametokana na kikao cha kusukuma mashauri kilichofanyika leo tarehe 28 Juni, 2023 katika Ukumbi wa Mahakama hiyo, kilichokuwa chini ya Mwenyekiti Mhe. Bernard Mpepo ambaye ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, ambacho kiliwahusisha wadau wa Haki Jinai.
Wadau hao ni Jeshi la Polisi Wilaya ya Babati, Ofisi ya Muendesha Mashtaka Mkoa wa Manyara, Mawakili wa Kujitegemea, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Huduma kwa Jamii pamoja Ofisi ya Magereza Mkoa wa Manyara.
“Inatubidi tuzidishe uhusiano wa ofisi zote za Mkoa wa Manyara zinazohusika na masuala ya Haki Jinai ili tuweze kuondoa mashauri ya mlundikano yaliyopo sasa na tuwe na mkakati wa kuzuia mlundikano usijitokeze hapo baadae,”amesema Mhe. Mpepo.
Katika kikao hicho, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Manyara ambazo ni Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto na Simanjiro wameelezea hoja zao kuwa upelelezi kutokukamilika mapema ni moja wapo ya mambo yanayochelewesha kesi kumalizika kwa wakati.
Mahakimu hao kwa pamoja wameazimia mashauri yote ya muda mrefu kuwa ifikapo Agosti, 2023 yawe yamekamilika.
Naye Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Manyara (RCO), Bw. Juma Majula amependekeza kuwa itafutwe njia rahisi ya mawasiliano baina yao, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali pamoja na Mahakama ambayo itasaidia kuwapata mashahidi kwa njia rahisi.
Aidha, upande wa TAKUKURU wamewashauri Mawakili wa Kujitegemea kutafuta namna ya kuwasiliana na wateja wao na kuwafundisha mambo yanayohusu sheria ili kupunguza malalamiko kwa sababu wateja wengi bado hawafahamu taratibu mbalimbali za Mahakama.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni