Na Faustine Kapama-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inashiriki Maonesho ya 47 ya
Biashara ya Kimataifa (SabaSaba) ili kutoa huduma na elimu kwa umma kuhusu
mambo mbalimbali ya kisheria, ikiwemo taratibu za kimahakama zinazolenga
kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi.
Ujenzi wa banda la Mahakama ambalo lipo mkabala na
lile la Jeshi la Kujenga Taifa katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya
Kilwa, Mkoa wa Dar es Salaam umeshakamilika na watumshi kutoka kurugenzi, idara
na vitengo mbalimbali wapo tayari kuanza kuwahudumia wananchi.
Katika maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania ipo katika
banda moja na baadhi ya wadau wake muhimu, wakiwemo Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Wadau wengine ni Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA),
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Shule ya Sheria kwa Vitendo
Tanzania na wengine, ambao wanatoa elimu ya sheria kwenye maeneo yao.
Tayari wananchi ambao wamefika katika banda hilo wameanza
kupatiwa huduma za kimahakama tangu jana, ikiwemo Mahakama Inayotembea kusikiliza mashauri
mbalimbali. Baadhi ya wananchi waliosikilizwa wamepongeza Mahakama kwa
kuanzisha huduma hiyo ambayo ni ya mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na
Dunia nzima.
“Bado sijaamini kama kesi yetu imesikilizwa, maana
tumechukua muda mfupi na sasa tunaenda kufanya mambo mengine. Huduma ya
Mahakama hii ni nzuri sana, kwani haki inapatikana kwa haraka na kwa wakati,
ingependeza kama itasambaa nchi nzima, ni mfano mzuri kwa Bara la Afrika na
duniani kote,” alizungumza mwananchi mmoja jana.
Huduma zingine zitakazotolewa na Mahakama katika
kipindi chote cha maonesho hayo ni kutoa elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani na safari kuelekea Mahakama Mtandao, 'e-Judiciary'.
Kadhalika, kuna utoaji wa elimu kuhusu huduma na
taratibu mbalimbali za ufunguaji wa mashauri, yakiwemo ya mirathi na utoaji wa
elimu kuhusu masuala ya ndoa, talaka, wosia na mirathi.
Wataalamu wa Mahakama pia wataelezea mfumo
ulioboreshwa wa kusajili, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa mashauri na
kuelezea huduma zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama, ikiwemo Divisheni
zake.
Katika kipindi hicho cha maonesho, kutakuwepo na utoaji
wa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja, ‘Call
Centre’ cha Mahakama ya Tanzania katika kutoa maoni na malalamiko na namna ya
kupata mrejesho.
Mahakama pia, kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto, itatoa fumu za udahili na kuzipokea zile ambazo zimeshafanyiwa kazi,
huku Chama cha Mawakili Tanyanyika kikiwa bega kwa bega kutoa msaada wa kisheri
kwa wananchi.
Zoezi la kutoa elimu masuala mbalimbali limeshaanza.
Kazi inaendelea, njoo banda la Mahakama tukuhudumie chap chap.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni