Ijumaa, 2 Juni 2023

JAJI MRISHA ATOA RAI KWA MAHAKIMU KUJIENDELEZA KITAALUMA; AWASIHI KUTOISAHAU TEHAMA

Na. James Kapele – Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakar Mrisha amewataka Mahakimu wa Kanda hiyo kujiendeleza kitaaluma ili kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali ya kisheria yanayofanyika ili kuwa na uelewa wa pamoja kwa watumiaji wa sheria hizo.

Akifungua mafunzo kwa Mahakimu jana tarehe 1 Juni, 2023 mkoani Katavi yenye lengo la kuwapitisha katika mabadiliko mbalimbali ya sheria ambazo wanazitumia katika majukumu yao ya kila siku, Mhe. Mrisha alisema ni vyema kuwa na ufahamu wa mambo mbalimbali yanayowezesha utekelezaji wa majukumu.

“Pamoja na juhudi hizi zinazofanywa na Mahakama katika kuwaelimisha hasa kwenye hizi sheria na kanuni na miongozo mbalimbali ni vyema pia na nyinyi mkajijengea tabia ya kujifunza kila siku ili kuendana na mabadiliko ya sheria zetu,” alisema Jaji Mrisha.

Aliongeza kuwa, hakuna anayejua kila kitu na hakuna aliye mkamilifu hivyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake kujifunza huku akisisitiza pia kujiendeleza kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa taaluma hiyo wanaweza kuitumia mahakamani kwa kuwa Mahakama inasisitiza matumizi ya Teknolojia.

Mafunzo  hayo ambayo yaliendeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde.

Akizungumza wakati akitoa mafunzo hayo, Mhe. Kasonde aliwaeleza washiriki kwamba, Sheria hizi ambazo Mahakama imekusudia kuwafundisha zimeshaanza kutumika na baadhi ya washiriki wamezitumia katika majukumu yao lakini Mahakama imeona ni vyema kuwapitisha katika maeneo ambayo yanahitaji ufafanuzi wa namna ya kuzitumia.

Kwa upande mwingine, washiriki wa mafunzo hayo wamefurahia na kuipongeza Mahakama kwa kuandaa mafunzo hayo na kwamba yamewapa uelewa wa pamoja katika mabadiliko ya sheria mbalimbali.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanganyika, Mhe. Glory Mwakihaba ameiomba Mahakama kujenga utamaduni wa kutoa mafunzo ya namna hiyo mara kwa mara kwa kuwa yanawajengea uwezo.

Mafunzo hayo yamelenga kuwapitisha Mahakimu katika sheria mbalimbali zikiwemo za Kanuni za Utaratibu wa madai madogo G.N 167/2023, Kanuni za Mawakili na Waendesha Mashtaka katika Mahakama za Mwanzo G.N 168/2013 na Sheria ya Madai Marekebisho ya jedwali la kwanza la Kanuni G.N 760/2023 ambapo amri ya VIII na XVIII zimerekebishwa kuruhusu kupokea Ushahidi wa shahidi kupitia maelezo yaani (Witness statement).

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakar Mrisha akifungua mafunzo kuwapitisha Mahakimu mkoani Katavi katika mabadiliko ya sheria  mbalimbali, mafunzo hayo yalitolewa jana tarehe 1 Juni, 2023 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde ambaye ndiye Mwezeshaji wa Mafunzo hayo. 

Katika picha ni sehemu ya Mahakimu waliohudhuria mafunzo wakifuatilia mada inayotolewa. Aliyeketi wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanganyika, Mhe.Glory Mwakihaba.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde (aliyesimama) akifafanua jambo katika mafunzo hayo. Kulia ni aji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakar Mrisha.

Picha ya pamoja ya Washiriki wa mafunzo hayo. Katikati ni Jaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakari Mrisha, wa pili kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde na wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanganyika, Mhe.Glory Mwakihaba.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni