Asifu uwepo wa Mahakimu wenye Mamlaka ya ziada katika undeshaji wa mashauri
Na Stephen Kapiga –Mahakama, Mwanza
Mahakama zilizopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Mwanza zimeendelea kuwakosha wananchi kwa kasi yake ya uondoaji mashauri kwa wakati na hivvo kuwawezesha kujikita katika shughuli za uzalishaji mali kuliko kutumia muda mwingi mahakamani kufuatilia kesi zao.
Akizungumza na mwakilishi wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano . cha Mahakama ya Tanzania, tarehe 1 Juni, mwaka 2023 Bi. Anna Kweba aliisifu Mahakama kwa kuwafikiria wananchi hasa wenye mashauri yao ya rufani Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwapa Mahakimu Mamlaka ya ziada na kusikiliza kesi zao.
“Nampongeza Mhe. Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na wenzake kwa busara hii ya kuongeza watu ambao wanasaidia upatikanaji wa haki zetu kwa wakati. Mimi natoka Ukerewe lakini tangu nimefungua rufaa yangu ya kesi ya ardhi haijafika hata mwezi lakini leo tumepata maamuzi ya shauri letu na hivo kutusaidia na kuondokana na safari za mara kwa mara kuja Mwanza kwa ajili ya kesi,” alisema Bi. Anna.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, Mhe. Monica Ndyekobora alisema kuwa haina haja ya kuchelewesha kutoa maamuzi ya rufaa hasa pale sababu za rufaa zinapokuwa zipo wazi na wadaawa wote wakiwa wapo.
“Tukiwa kama Mahakimu wenye Mamlaka ya ziada tuna jukumu la kusaidia kasi ya uondoaji wa mashauri hasa pale Mahakama Kuu ya Tanzania inapokuwa imezidiwa na wingi wa mashauri. Kwa hiyo huna haja ya kukaa na shauri muda mrefu ikiwa unaweza kuwaskiliza wahusika na jukumu letu kubwa ni kutoa maamuzi kwa kuzingatia sheria na sio kuhahirisha mashauri” alisema Mhe. Monica.
Aidha kwa mujibu wa takwimu za kikao cha menejimenti kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei 2023 jumla ya mashauri 1,226 yamefanyiwa maamuzi ndani ya Mahakama zilizopo ndani ya kituo hicho. Kituo hicho, kinajumisha Mahakama ya Mwanzo Buswelu, Mahakama ya Wilaya Ilemela, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza pamoja na Masjala ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Katika kipindi cha Desemba 31, 2022 kituo hicho kilibaki na mashauri 1,232 na kwa kipindi cha Januari hadi Mei 2023 jumla ya mashauri 1,011 yalifunguliwa na jumla ya mashauri 1,226 yametolewa maamuzi na kufikia Mei 31 mwaka 2023, wakati mashauri 982 tu ndio yanayoendelea na kufanya kituo hicho kuwa kasi kubwa ya viwango vya uondoshaji wa mashauri yake kwa asilimia 121.3 na huku kasi ya umalizaji asilimia 54.
“Mafanikio haya ya kasi ya uondoaji wa mashauri imechagizwa zaidi na ushirikiano uliopo baina ya wadau wote wa Mahakama kuanzia Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu, Mawakili, Waendesha Mashitaka, Wadaawa na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla. “Mafanikio haya hayajatokea tu hivihivi bali ni kutokana na kuwa na mipango madhubuti ya kuthibiti ile tabia ya baadhi ya Mawakili au Wadaawa kwa kufanya Mahakama sehemu ya kupaki kesi zao na kushindwa kuzifuatilia mwendelezo wake.
“Lakini kutokana na kila mmoja kuweza kujua wajibu wake ndio maana leo hii tunayaona mafanikio haya ingawa kwetu bado tupo kwenye safari zaidi ya kufikia malengo yetu ya kufunga mwaka wa 2023 tukiwa na kesi chini ya 400 katika kituo hiki jumuishi cha utoaji haki,”alisisitiza Monica .
Kituo cha IJC mkoani Mwanza kilianza rasmi shughuli zake katika eneo la Buswelu mkoani Mwanza mwezi Mei 2022, ambapo mpaka kufikia sasa ni mwaka mmoja umetimia na wananchi wameanza kuona matunda ya utendaji kazi wake.
Hakimi Maze Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe. Monica Ndyekobora(aliyevaa mewani) akiwa katika kikao cha menejimenti kilichokuwa kinazungumzia kasi ya uondoshaji wa mashauri katika Kituo Jumishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoa wa Mwanza.
Baadhi ya wajumbe wengine wakiwa katika kikao hicho.
( Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni