Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewatoa hofu Majaji kuhusu
ujio wa mfumo mpya wa kielektroniki ulioboreshwa utakaoanza kutumika hivi
karibuni kwani unaenda kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili
mifumo iliyopita katika kuratibu mashauri mahakamani.
Akizungumza kwenye awamu
ya pili ya Majaji wa Mahakama Kuu wanaoshiriki kwenye mafunzo kuhusu mfumo huo
wa ‘advanced e-case management system’ katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania
jijini Dar es Salaam leo tarehe 5 Julai, 2023, Mhe. Siyani amesema kila kitu
kitaendelea kufanyika kama ilivyo siku zote.
“Tunapoanza kitu kipya
huwa tunakuwa na hofu, hofu ni kitu cha kawaida wakati wowote ule unapoanza
kitu kingine, hofu ni sehemu ya maisha yetu. Watalaam wetu wapo na mimi
niwaombe muondoe hizo hofu ili mkiondoka kwenye chumba hiki muwe na amani kwamba
kila kitu kitaendelea kama tulivyokuwa tunafanya siku zote,” amesema.
Jaji Kiongozi ameeleza matumaini
yake kuwa mfumo huo watakapoanza kuutumia utakuwa na tija nyingi ambazo
zinajaribu kujibu maswali au changamoto za mifumo iliyopita, ikiwemo JSDS1 na
JSDS2 ambayo ilikuwa na changamoto mbalimbali na Majaji hawakuhusishwa kwa
kiasi kikubwa.
“Kwa sasa tunatoka
kwenye JSDS2 tunaenda kwenye ‘advanced case management system’ ambayo imetatua changamoto
zilizokuwepo kwenye mifumo iliyopita, ikiwemo kuelemewa na uzito wa nyaraka,
kushindwa kuhifadhi kumbukumbu za mienendo ya mashauri na kadhalika,” amesema.
Mhe. Siyani amebainisha
kuwa mfumo huo wa sasa unaoanishwa na mifumo mingine utasaidia kuondoa
tatizo kuhusu kumbukumbu za Mahakama na kuleta faida zingine nyingi, ikiwemo kurahisisha
upandishaji wa moja kwa moja maamuzi kwenye kanzi data zingine kama TanzLii badala
ya kupitia kwa wasaidizi wao.
Amewapongeza watalaam kutoka
Kurugenzi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliamno (TEHAMA) na Usimamizi wa Mashauri
kwa kufanya kazi kubwa ya kujenga mfumo huo na kuwaomba Majaji kuwa vinara wa kuutumia
utakapoanza kufanya kazi na wasirudi nyuma.
“Sisi ni viongozi, tukirudi
nyuma hatutafanikiwa, hatutatoka hapa tulipo, lazima tuchukue nafasi zetu ili
kuwafanya wale waliochini yetu nao wahame kutoka kwenye matumizi ya karatasi
kwenda katika teknolojia. Tukifanikiwa tutakuwa tumeweka kumbukumbu sawa kwa
wenzetu wengine kufuata, siyo tu hapa nchini lakini pia nje ya nchi yetu,” amesema.
Mhe. Siyani amesema Mahakama
ya Tanzania inapaswa kujivunia kwa maboresho makubwa yaliyofanyika na
yanayoendelea kufanyika, ikiwemo ujenzi wa mfumo huo mpya unaolega kurahisisha
shughuli za utoaji haki mahakamani.
“Sisi tunaopata nafasi
ya kukutana na wenzetu kwenye mataifa yaliyoendelea kujifunza wanafanyaje, utaona
tunaweza kuwa maskini kwenye vitu vingine, lakini katika namna ambavyo
tunakwenda na ukiwasikiliza utaona sisi tumepiga hatua zaidi kuliko wao na tunao
uwezo wa kuonyesha njia, tunakoelekea ni kuzuri zaidi,” amesema.
Amewakumbusha Majaji
kuwa ujenzi wa mfumo ni mchakato, hivyo wakikumbana na changamoto kadhaa wakati
wa kuutumia wasisite kutoa maoni, kwani ndiyo yatakayosaidia kuufanya siku moja
uwe mzuri unaoridhisha kwa kila mmoja.
“Huu mfumo wa kielektroniki
utatuwezesha na kurahisisha kazi zetu za usikilizaji wa mashauri. Ujenzi wa
mfumo ni hatua, haukamiliki siku moja. Mtakapokuwa mnapitishwa mtaendelea kuona
changamoto,” Jaji Kiongozi amesema.
Ameeleza kuwa mfumo huo umeanza
kujengwa tangu mwaka jana na kuna wengine walishatoa maoni mbalimbali, hivyo na
wao watakapopitishwa wanaweza kuona maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa. Mhe.
Siyani amewaomba watalaamu waliopo kuendelea kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha
mfumo huo.
Awali akitoa neno la
utangulizi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema mafunzo
hayo yatafanyika kwa Majaji wote wa Mahakama Kuu katika makundi matatu, lengo ni
kuwapa uelewa wa mfumo huo wa advanced case management system, kwa vile wao ni
miongoni mwa watumiaji wakubwa.
Alieleza kuwa ujenzi wa
mfumo huwa ni endelevu, kwa maana huhitaji kuboreshwa kila siku, hivyo
wanategemea wakati wa mafunzo kupata mrejesho kutoka kwa Majaji kwenye maeneo
ya kufanyia maboresho.
“Tunatambua kuwa kuna
yale ambayo yataweza kufanyiwa kazi mara moja wakati hatujaanza kuutumia mfumo
na mengine yatafanyiwa kazi wakati matumizi yake yakiendelea,” amesema, huku akibanisha
kuwa ni jambo la kujivunia kwa vile mfumo huo umejengwa na watalaamu wa ndani
ya Mahakama ya Tanzania.
Mahakama ya Tanzania inafanya
maboresho ambayo yalianza siku nyingi hatua kwa hatua tangu mwaka 1980, lengo ni
kuhakikisha huduma za utoaji haki zinapatikana kwa kutumia teknolojia kwa
matumanini kwamba yatarahisisha zaidi kazi za utoaji haki kwa wananchi.
Kufanyika kwa mafunzo
kuhusu mfumo huo mpya ni mwendelezo wa yale yaliyotolewa kwa Majaji wa Mahakama
ya Rufani na kundi la kwanza la Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika
ukumbi huo hivi karibuni. Mafunzo hayo yalifunguliwa kwa mara ya kwanza na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni