- Jaji Mfawidhi akiri vikao hivyo vimesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri
Na Elisia Meela, Mahakama Kuu Dar es Salaam
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inaendelea kufanya vikao na wadau wake lengo ni kusukuma mashauri ya madai ili kuondokana na uwepo wa mashauri ya muda mrefu (Backlog) yaliyopo katika Kanda hiyo.
Akizungumza hivi karibuni na wadau hao, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alisema vikao hivyo vimesaidia kuondosha mashauri kwa asilimia kubwa.
“Kumekuwa na matokeo mazuri ya kikao maalum cha kusukuma mashauri kilichofanyika kuanzia tarehe 15 Mei, 2023 mpaka 15 Juni, 2023 kwa kuhusisha Majaji wa Mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam na Majaji kutoka nje ya Dar es Salaam. Kikao hicho kilifanikiwa kwa asilimia 90,” alisema Mhe. Maghimbi.
Jaji Mfawidhi huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao aliwaeleza wadau juu ya mipango iliyopo kuhusu mashauri ya madai ambayo ni ya muda mrefu kuwa yameshatambuliwa na kuainishwa na tayari maandalizi ya vikao maalum vya kuyasikiliza yanafanyika.
Hata hivyo, katika kikao cha Madalali miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na changamoto wanazokutana nazo Madalali katika kutekeleza majukumu yao.
Hata hivyo, Mahakama iliwahakikishia wajumbe (Madalali) kuwa kwa kuzingatia changamoto wanazopitia, Mahakama Kanda ya Dar es Salaam itatoa elimu kwa wadau wengine ili kuondokana na changamoto hizo na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake.
Kadhalika, katika kikao cha kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na katika kikao cha ‘Bench bar’ ajenda ilikuwa ni majadiliano kuhusu mikakati iliyowekwa na Mahakama ili kuondosha mashauri yaliyokaa muda mrefu (backlog) kwa kuandaa vikao maalum vya kusikiliza mashauri hayo.
Katika kikao hicho, Mhe. Maghimbi aliwasihi wajumbe kutoa ushirikiano katika kutekeleza maazimio ya kuondosha mashauri ya muda mrefu mahakamani.
Wajumbe waliohudhuria katika vikao hivyo ni Mawakili wa kujitegemea wakiwakilisha chapta za Mkoa wa Dar es salaam na Pwani na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni