Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Mawakili wapya kubadilika kifikra, kimitazamo
na mbinu za utoaji wa huduma ili kuziona fursa za ajira ambazo zinaibuliwa
katika karne ya sasa.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito
huo leo tarehe 6 Julai, 2023 katika sherehe ya 68 ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili
wapya 195 iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Tukio
hilo linafanya kwa sasa Mawakili kufikia 11,637.
“Mkiganda katika zama iliyopita,
zama inayotokana na aina ya masomo tunayopata Chuo Kikuu, aina ya masomo
tunayopata kupitia Shule ya Sheria tutakosa hizo fursa na pengine tutabaki watu
ambao tunalalamika mara kwa mara,” amesema.
Jaji Mkuu amesema kuwa umefika
wakati Mawakili na Wanasheria Vijana kukubali ukweli kuwa Elimu ya Sheria waliyopata
Vyuo Vikuu na Shule ya Sheria, haikuwatayarisha kukabiliana na changamoto ya
kutafuta fursa zinazoibuliwa na mabadiliko katika Karne ya 21.
Amesema ni vizuri kwa
Mawakili hao kujiweke katika hali ya kusoma fursa katika mabadiliko mbalimbali
ambayo yanatokea katika jamii na wasipoelewa dunia ambayo inawazunguka hizo fursa
hawataziona wala kuwafuata nyumbani kama ilivyokuwa zamani.
Mhe. Prof. Juma
amesisitiza kuwa Mawakili wanatakiwa kuwa na miwani ambayo ni tofauti na miwani
waliyoizoea, miwani ambayo itaweza kuona fursa ambazo watu wengine hawazioni.
“Mawakili wapya hamuwezi
kuziona fursa mpya za karne ya 21, kama mitazamo yenu, tamaduni na uelewa wenu
wa sheria ni kupitia miwani na maudhui ya dunia ya karne za 19 na 20,” amesema
Jaji Mkuu.
Amesema huwa anafuatilia
mijadala katika mitandao ya kijamii, kwa bahati mbaya amegundua bado Wanasheria
na Mawakili wa Tanzania wanajenga hoja zao kwa kutumia uoni na miwani ya zamani
isiyoweza kuona fursa zilizozalishwa na utandawazi na ukuaji mkubwa wa matumizi
ya teknolojia.
Jaji Mkuu amebainisha
pia kuwa Wanasheria na Mawakili bado hawajaweza kuona fursa kubwa tarajiwa
kutoka kwenye miradi mikubwa ya kiuwekezaji, mfano Reli ya Kisasa ya Mwendokasi
(SGR) na Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, ambazo zinalenga kufungua
fursa za ajira sio tu ndani ya Tanzania, bali pia nchi zingine katika Bara la
Afrika.
“Juzi nilikuwa Namibia,
nikaongea na Mawakili wa huko, wao ujenzi wa SGR ni fursa na wanaanza kuangalia
ni namna gani watakuja kutoa huduma hapa Tanzania. Wanaposikia kuwa kuna bwawa
kubwa la umeme ambalo litaibua viwanda, wao kama Mawakili wanasema kwao ni fursa
ambayo itawaunganisha Tanzania na nchi zingine za kiafrika,” amesema.
Hivyo, amewaomba
Mawakili hao kujibadilisha wao wenyewe na kujiendeleza kwa kuvaa miwani yenye
uwezo wa kuona hizo fursa. Alitoa mfano wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Hayati Benjamin William Mkapa katika kitabu chake cha “My Life My Purpose’’
katika ukurasa 96.
Alimnukuu Rais Mstaafu akisema,
“We Must Change Ourselves or We Will Be Changed,’’ maana yake ni kwamba, “Ni
Lazima Wanasheria na Mawakili Tujibadilishe kifikra, kimtazamo na kinyakati, vinginevyo
tutalazimishwa kubadilika.’’
“Tunayo nafasi sisi
vijana ambao tuna muda mrefu zaidi wa kutoa huduma, usitegemee sana Mawakili ambao
tayari wanazo ajira, hawatawazungumzia sana, nyinyi ndiyo mnatakiwa kuibua hizo
fursa, kwa sababu wale ambao wanazo hawatakuwa na nia ya kuongelea changamoto
ya ajira ambayo inawakumba Mawakili wanaoingia katika soko la ajira,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
pia kuwa katika miaka ya hivi karibuni, masuala yanayozungumziwa katika
Mikutano ya Jukwaa ya Majaji Wakuu wa Nchi za Afrika Kusini na Mashariki ya
Afrika ni kielelezo tosha kuwa Mahakama Barani Afrika zimeamua kubadilisha
fikra na mitazamo.
Amesema hiyo inafanyika kukabiliana
na changamoto zinazokabili nchi zetu katika Karne ya 21 ambazo ni tofauti na
changamoto zilizokuwepo kuanzia miaka ya uhuru 1960 hadi ya Karne ya 21
iliyoanza tarehe 1 Januari, 2000.
Hivyo, amewasihi
Mawakili wapya kwenda kupima miwani mipya ili waweze kuona fursa za kiushindani
nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndani ya Eneo Huru la Biashara la
Bara la Afrika (African Free Trade Area (AfCFTA).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni