Na Christopher Msagati-Mahakama, Manyara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Manyara, Mhe. John Kahyoza amesisitiza
watumishi katika Kanda hiyo kwenda na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ulimwengu uliopo sasa.
Mhe
Kahyoza ametoa msisitizo huo leo tarehe 06 Julai, 2023 wakati wa mafunzo ya ndani
yaliyokuwa yanatolewa kwa watumishi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi
Manyara, Mahakama ya Wilaya Babati na Mahakama za Mwanzo zilizopo Babati.
“Teknolojia
inakwenda kwa kasi sana na kwa hakika hatujui huko mbeleni miaka ijayo kitu
gani kitatokea, hivyo ni rai yangu kwenu watumishi kujitahidi kwenda na mabadiliko
hayo kwa sababu hatuna namna ya kuyaepuka katika kazi zetu, ni lazima tutumie
TEHAMA,” amesema.
Mafunzo
hayo ya ndani yalihusu matumizi ya E-Office na matumizi mengine ya kimtandao
katika shughuli za Mahakama, utunzaji wa kumbukumbu unaozingatia viwango pamoja
na utunzaji wa nyaraka pamoja na kutunza siri. Bw. Damasi Axwesso, Fatina
Haymale na Christopher Msagati ambao ni watumishi wa Mahakama ndiyo waliokuwa
watoa mada katika mafunzo hayo.
Katika
hatua nyingine, mtumishi Happyness Mungure alitumia nafasi hiyo kuwajulisha watumishi
wengine masuala ambayo yalijiri kwenye Baraza la Wafanyakazi ambalo lilifanyika
Dodoma mwezi Juni, 2023.
Mahakama
Kuu Kanda ya Manyara imejizatiti katika kutoa mafunzo mbalimbali ya mara kwa
mara kwa watumishi wake ili kuboresha utendaji wao wa kazi pamoja na ufanisi
ambao utaleta tija katika utoaji huduma za kimahakama.
Mtoa mada, Bw. Damasi Axwesso akitoa mada kwa watumishi wenzake wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni