Jumanne, 4 Julai 2023

JAJI POMO ATEMBELEA GEREZA LA UBENA

·Afanya ukaguzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya Kibaha

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Musa Pomo, akiongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe.  Joseph Luambano, jana tarehe 3 Julai, 2023 alitembelea Gereza la Ubena na kuongea na wafungwa na mahabusu.

Akiwa katika Gereza hilo, Mhe. Pomo alipokea taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Gereza, Mrakibu wa Magereza Godwin Mekoki ambaye alibainisha kuwa Gereza hilo lilianzishwa mwaka 1964 na mpaka sasa lina askari 91, wafungwa na mahabusu 214.

Mkuu wa Gereza pia alieleza changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo umbali kutoka katika Gereza hilo na Mahakama ya Wilaya Bagamoyo na usafiri ambao siyo rafiki wanaotumia kubeba mahabusu.

Kadhalika, Mhe. Pomo alipokea risala fupi iliyoandaliwa na mahabusu na wafungwa ambao waliomba nakala za hukumu kutolewa kwa wakati ili waweze kukata rufaa kwa wakati.

Walieleza jinsi wanavyochelewa kuitwa Mahakama Kuu kusikiliza mashauri mbalimbali, ikiwemo ya mauaji baada ya upelelezi kukamilika. Pia waliomba upande wa mashtaka kuleta mashahidi kwa wakati ili kesi zimalizike mapema na kujua hatima zao.

Hoja hizo zilijibiwa na baadhi ya viongozi wa Mahakama walioambatana na Mhe. Pomo kwenye ziara hiyo. Viongozi hao ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Samira Suleiman. Katika ziara hiyo walikuwepo pia wadau wa haki jinai.

Akijibu hoja ya kuchelewa kuitwa Mahakama Kuu, Naibu Msajili alisema kesi hizo tayari zimepangiwa tarehe kwenye kalenda ya Mahakama kwenye vikao vilivyopangwa, hivyo mahabusu wanaohusika wataitwa muda sio mrefu.

Kuhusu nakala za hukumu, Mhe. Samira alisema zilichelewa kupatikana kutoka na tatizo la umbali, ila tangu jana zimeshafikishwa katika ofisi ya magereza.

Aidha, kuhusu suala la upelelezi kuchelewa, alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bagamoyo hivi karibuni imeitisha majalada yote ya jinai na kuyapitia ili kujiridhisha kama mashtaka yana msingi wa kuendelea ama kuondolewa.

Majibu hayo yaliungwa mkono na Mkuu wa Mashtaka Chalinze, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bi. Janeth Magoho ambaye alisema tayari zoezi hilo limeshakamilika na majibu yatapatika kwa tarehe husika ya kesi.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Pomo na wadau wa haki jinai Mkoa wa Pwani walipata fursa ya kutembelea zahanati ya Gereza inayohudumia familia za askari, wafungwa, mahabusu na raia na kujionea miundombinu iliyopo. Walitembelea pia jiko la Gereza hilo na kushuhudia chakula kilichopikwa na wafungwa na baada ya kuonja walikisifia chakula hicho kilivyokuwa kitamu.

Mhe. Pomo pia alifanya ukaguzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha na kuagiza uwepo wa taarifa ya ukaguzi wa mara ya mwisho ili kujiridhisha kama yale makosa yaliyofanyika mwanzo yamerekebishwa. Kadhalika, alitaka kujua namna changamoto zimetatuliwa ili zisiendelee kujirudiarudia.

Akiwa katika Mahakama hizo, Jaji Pomo alipokea taarifa ya nusu mwaka ya Mahakama Pwani kutoka kwa Mhe. Mkhoi ambaye alisema matumizi ya Mahakama mtandao yamekuwa na ufanisi mkubwa katika Mkoa wa Pwani kwani yamepunguza msongamano wa mahabusi ambao kesi zao ziko katika hatua ya awali ya kutajwa na zile zenye mashahidi walioko mbali.

Baada ya ukaguzi huo, Mhe. Pomo alipata fursa ya kuongea na baadhi ya watumishi waliokuwepo ofisini na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya kuikuza taasisi, kwani hata wakistaafu wataacha kumbukumbu nzuri kwa vizazi vijavyo.

 



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Musa Pomo akiwa na Mkuu wa Gereza la Ubena, Mrakibu wa Magereza Godwin Mekoki alipotembelea Gereza hilo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Musa Pomo (katikati) akiwa nje ya Gereza na wadau wa haki jinai Pwani. Waliosimama mbele ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.  Joseph Luambano (wa pili kushoto), Mkuu wa Gereza la Ubena, Mrakibu wa Magereza Godwin Mekoki ( wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi ( wa pili kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Samira Suleiman ( wa kwanza kulia).

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Musa Pomo ( katikati aliyesimama) akizungumza na watumishi (picha chini). Kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.  Joseph Luambano na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi. 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni