Na. Paul Pascal-Mahakama, Moshi.
Majaji sita wa Mahakama ya
Rufani wameanza kusikiliza jumla ya mashauri 65 kwenye vikao maalumu vinavyofanyika
katika Mahakama Kanda ya Moshi.
Akizungumza wakati wa
kuanza vikao hivyo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mhe.
Emmanuel Mrangu amesema kutakuwepo na Majopo mawili ya Majaji hao yanayoongozwa
na Mhe. Mwanaisha Kwariko na Mhe. Winfrida Korosso.
"Katika jopo la
kwanza, Mhe. Kwariko atakuwa pamoja na Mhe. Dkt. Mary Levira na
Mhe. Gerson Mdemu ambalo litasikiliza mashauri 32, huku katika jopo la pili, Mhe.
Korosso atakuwa pamoja na Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Mhe. Sam Rumanyika ambalo
litasikiliza mashauri 33," amesema Mhe. Mrangu.
Alisema vikao hivyo
vitakaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwenye kumbi za wazi namba moja
na namba mbili kusikiliza mashauri hayo 65 ambayo kati ya hayo 49 ni rufaa za
madai na 16 ni rufaa za jinai. Vikao hivyo vitakaa kwa muda wa wiki tatu
kuanzia July 3, 2023.
Mhe. Mrangu amesema lengo
la kuleta vikao hivyo katika Mahakama Kanda ya Moshi ni utekeleza wa Mpango
Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2020/21-24/25) nguzo ya pili ya upatikanaji wa
haki kwa wakati.
"Hii itawasaidia
wananchi kupata haki zao kwa wakati badala ya kusubiri muda mrefu kama ilivyokuwa
awali ambapo mashauri yalikuwa yanapelekwa Mahakama Kanda ya Arusha na Dar es
Salama,” alisema.
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni