Jumanne, 4 Julai 2023

WATUMISHI MAHAKAMA KANDA YA BUKOBA WAPEWA MREJESHO WA MKUTANO BARAZA KUU

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi, hivi karibuni aliongoza ujumbe wa viongozi waliohudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Dodoma kutoa mrejesho wa kilichozungumzwa na maazimio yaliyofikiwa.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba kilihudhuriwa pia na viongozi wa Mahakama hiyo, wakiwemo Majaji, Kaimu Naibu Msajili, Mhe. Janeth Massesa na Mtendaji, Bw. Lothan Simkoko

Baada ya kufungua Kikao hicho, Mhe. Banzi alianza kwa kuwasalimia wajumbe wa kikao kwa salamu ya Mahakama kwa kusema “Mahakama ya Tanzania” na wajumbe kuitikia “Uwajibikaji, Weledi, na Uwadilifu.” Baada ya salamu hiyo alimkaribisha Mtendaji wa Mahakama kutoa taarifa fupi ya mrejesho wa Baraza Kuu la Wafanyakazi lilofanyika Dodoma kuanzia tarehe 18-19 Mai, 2023.

Bw. Simkoko aliwapitisha wajumbe kwa ufupi kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Baraza Kuu, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahimu Juma.

Alieleza umuhimu wa Baraza Kuu ambalo hujadili stahiki za wafanyakazi, maboresho yanayoendelea mahakamani, ujenzi wa Mahakama ppya, maslahi ya watumishi pamoja na matumizi ya Technolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Bwa. Simkoko alisisitiza mwendelezo wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA mahakamani ikiwemo JSDS II, e-Wakili, Tanzlii, Judicial Mail, e-Malalamiko pamoja na mfumo mpya unaotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni wa Advanced Case Management Systems (e-CMS).

Aliendelea kuelezea hoja nyingine zilizozungumziwa kwenye Baraza Kuu na kupatiwa ufumbuzi, ikiwemo uhaba wa watumishi, madai ya malimbilizo ya mishahara, mafunzo kwa watumishi, suala la kikokotoo, upandishwaji wa madaraja pamoja na posho ya mavazi.

Akihitimisha kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwakumbusha watumishi wote wa Kanda hiyo kuepuka vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili ya utumishi wa umma na kusisitiza umalizaji wa mashauri kwa wakati na kutokuahirishapasipokuwa na sababu za msingi.

Jaji Mfawidhi na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi (katikati) akisisitiza jambo. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Emmanuel Ngigwana na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Monica Ottaru.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko akiwasilisha taarifa fupi ya mrejesho wa Baraza Kuu la Wafanyakazi lililofanyika Dodoma.  

Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Bukoba (juu na picha mbili chini) wakimsikiliza Jaji Mfawidhi na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi (hayupo pichani).

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni