Na Faustine Kapama-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inapaswa
kujivunia kwa maboresho makubwa yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika, ikiwemo
ujenzi wa mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu mashauri kama sehemu ya
kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), unaolega kurahisisha
shughuli za utoaji haki mahakamani.
Hayo yamebainishwa na Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani leo tarehe 3
Julai, 2023 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam
alipokuwa anawakaribisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kushiriki kwenye mafunzo
ya siku mbili kuhusu mfumo huo mpya ulioboreshwa (advanced e-case management).
“Mahakama imekuwa kinara,
inawezekana sisi wenyewe tupo humu ndani hatujifanyii tathmini na kutambua ni
kwa kiasi gani tumepiga hatua katika matumizi ya TEHAMA, lakini tunaopata fursa
ya kuwa na wadau wetu mbalimbali, ndani na nje ya nchi tunatambua hatua kubwa
tuliyofikia,” amesema.
Jaji Kiongozi amebainisha
kuwa mfumo huo wa 'e-case management,' pamoja na mambo mengine, umekusudia kurahisisha
kazi ya utoaji haki, ikiwemo kuwatoa kwenye kunukuu ushahidi na mienendo yote
kwa mkono na kuwaleta katika mfumo wa kisasa ambao teknolojia itafanya kazi
hiyo kwa niaba yao.
“Tunakoelekea ni kule
ambako teknolojia itatumika zaidi kwenye kazi ya utoaji haki nchini, badala ya
kumtegemea Jaji kuandika kila kitu kwa masaa mengi, kwanza kusikiliza, kutafsiri
na kisha kuandika,” amesema huku akipongeza jitihada zilizofanywa na Kurugenzi
ya TEHAMA na Usimamizi wa Mashauri na timu nzima inayoshughulikia masuala ya
ujenzi wa mifumo kwa kukamilisha mfumo huo mpya.
Mhe. Siyani amesema kuwa
kukamilika kwa ujenzi wa mfumo huo, angalau kwenye hatua hiyo iliyopo hivi sasa,
ni moja ya mafanikio makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania inapaswa kujivunia
inapopiga hatua kuelekea katika matumizi kamili ya TEHAMA kwenye utoaji haki.
“Tunaweza kufikiri kuwa
ni kitu kidogo, lakini ujenzi wa mifumo siyo kitu chepesi, kutoa mawazo na
kuyapeleka kuwa yenye kufaa kwenye akili bandia. Kwa asili ya kazi yetu inahitaji
kuelewa ule mchakato wa kazi za Mahakama unafanyaje kazi na mchango wa wadau
wetu,” amesema.
Amesema ni wazi mfumo wa 'e-case management' utasaidia kutatua changamoto na mapungufu mbalimbali ambayo yalikuwa
yanakabili mifumo mingine iliyopita, ikiwemo JSDS2. Ametaja mambo machache
ambayo mfumo huo utarahisisha shughuli za utoaji haki mahakamani tofauti na
iliyokuwa kwa mifumo ya zamani.
Jaji Kiongozi amesema mfumo
huo mpya utarahisisha ubebaji wa nyaraka, ikiwemo mienendo yote ya mashauri tofauti
na JSDS2 ambao ulionekana kuwa umeelemewa na uzito wa nyaraka na ulikuwa hauhifadhi
kumbukumbu za kutosha.
“Mfumo huu kwa sababu umeoanishwa
na mifumo mingine, ikiwemo e-Wakili utasaidia kuwatambua Mawakili vishoka na
pia kuondoa kadhia kubwa sana ambayo kila Jaji anaijua ya kupata kumbukumbu pale
ambapo tunasikiliza rufaa au wakati wa kufanya mapitio,” amesema.
Mhe. Siyani amebainisha
pia kuwa mfumo huo utarahisisha uitishwaji wa kumbukumbu kutoka kwenye Mahakama za chini ili kuwawezesha
Majaji kufanya maamuzi, kwa maana utakapokuwa umetumika kwenye ngazi
zote, mafaili yatapatikana kielektroniki kwa kutumia mfumo huo.
Amesema mfumo huo mpya utasaidia
kuondokana na changamoto ya kupakia hukumu kwenye mifumo mingine ya kuhifadhia
baada ya kumaliza kuandika na pia kuruhusu mienendo ya mashauri kuandikwa moja
kwa moja na kurahisisha uandishi wa hukumu kupitia kiolezo maalumu na kisha
kutuma moja kwa moja katika mfumo wa maktaba mtandao.
“Maboresho makubwa ya
mfumo huu yamejikita zaidi katika kurahisisha usajili wa mashauri kwa njia ya
mtandao kupitia nyaraka pepe za kimahakama, upangaji wa mashauri kwa Majaji na
Mahakimu, usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao pamoja na mambo mengi
kadha wa kadha,” Jaji Kiongozi amesema.
Kadhalika, Mhe. Siyani
amesema kutakuwa na urahisi wa Mahakama kusomana na mifumo ya wadau wake muhimu,
wakiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA), Magereza, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS),
pamoja na wengine, hivyo kurahisisha kupata taarifa mbalimbali.
Kufanyika kwa mafunzo kuhusu
mfumo huo mpya ni mwendelezo wa yale yaliyotolewa kwa Majaji wa Mahakama ya
Rufani katika ukumbi huo hivi karibuni. Mafunzo hayo yalifunguliwa na Jaji Mkuu
wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni