Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama ya Kazi
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina hivi
karibuni aliwaongoza Viongozi na watumishi wa
Mahakama hiyo kupata elimu ya uraia
na usalama barabarani iliyotolewa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Faustina
Ndunguru.
Afande
Ndunguru kutoka Kituo cha Polisi cha Usalama Barabarani Makao Makuu Dar es
Salaam aliwaasa madereva na watumiaji wa barabara kutoka Mahakama hiyo kufuata
sheria za barabarani na kupunguza makosa ya kibinadamu kwa kuacha kutumia
vyombo vya moto vilivyo chakavu.
Alihimiza
abilia wanapokuwa safarini kufunga mikanda na kuwaomba Viongozi kuwaanda
madereva wao kabla ya kuanza safari za mbali kwa kuwapa muda wa kutosha
kupumzika.
“Madereva
wanatakiwa kuwa makini na vyombo vya moto wanavyovitumia kwa kuhakikisha kila
kifaa kipo katika mfumo wake wa kawaida,” alisisitiza. Afande Ndunguru alibainisha
madhara ya ajali kuwa ni vifo, ulemavu, kupoteza ajira, kuharibika kwa chombo
na kupoteza familia.
Alieleza
njia za kukabiliana na ajali za barabarani kama kuacha ulevi na uzembe,
kuzingatia alama za usalama barabarani zilizowekwa, kupunguza msongo wa mawazo
na dereva kupumzika pale anapokuwa amechoka.
Akizungumza
baada ya kipindi hicho, Jaji Mfawidhi alishauri wasimamizi wa barabara
wanapotoa mafunzo kwa madereva washirikishe na wenza wao ili kupunguza tatizo
la msongo wa mawazo kwa dereva anapokuwa kazini.
Akiahirisha
mafunzo hayo, Jaji na Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Elimu katika Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo alimshukuru Afande Ndunguru kwa
elimu nzuri aliyoitoa na kufafanua jinsi gani makosa ya kibinadamu yanavyoweza
kusababisha ajali nyingi barabarani.
Mafunzo
hayo yalihudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Divisheni hiyo, Mhe.
Biswalo Mganga, Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Said Ding’ohi, Naibu Msajili, Mhe.
Enock Matembele na Kaimu Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Jumanne Muna.
Divisheni hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wadau wake kwa siku ya Jumatatu na Jumatano asubuhi na vile vile kuwezesha watumishi wake kupata elimu kwa mada mbalimbali siku ya Ijumaa.
Picha
ya Meza Kuu na baadhi ya Madereva wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Picha
ya Meza Kuu na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni