Jumanne, 22 Agosti 2023

‘IJC’ TEMEKE YAKUTANA NA WADAU; WAJADILI NAMNA BORA YA KUSHUGHULIKIA MALIPO YA MIRATHI

Na Mary Gwera, Mahakama

Uongozi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke umekutana na Wadau wake muhimu ili kujadili namna bora ya kuboresha zaidi ushughulikiaji wa malipo ya mirathi ili haki kwa wanufaika iweze kupatikana kwa wakati.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita na Wadau walioalikwa katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alisema lengo ni kukubaliana na kuweka sawa taratibu mbalimbali za ushughulikiaji wa malipo ya mirathi.

“Lengo la kuwaita hapa leo, ni pamoja na kufahamiana na kujadiliana namna nzuri zaidi ya kushughulikia malipo ya mirathi ili kutoa huduma bora kwa wateja wetu kwa wakati,” alisema Mhe. Mnyukwa.

Alisema wamewaita wadau hao ili kuwaelimisha zaidi kuhusu taratibu za ufunguaji, uendeshaji na ufungaji wa mashauri mbalimbali yanayofunguliwa katika Mahakama hiyo.

Aliongeza kuwa, kila mtu kwa wakati wake ni mteja mtarajiwa na Mahakama hiyo hivyo ni muhimu kuweka sawa mazingira ya ushughulikiaji wa mashauri hayo.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alisema kikao hicho, ni nafasi kwa wadau hao kutoa maoni yao na changamoto zinazowakabili ili kuona namna bora zaidi ya kuboresha huduma kwa wanufaika wa mirathi

Katika kikao hicho kilichoshirikisha Wadau kutoka Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, Magereza, Wizara ya Fedha pamoja ‘PSSSF’ waliazimia mambo kadhaa ambayo ni pamoja na kutolewa kwa elimu kuhusu taratibu za malipo ya mirathi na aina ya mafao kwa watumishi wa Majeshi.

Aidha; iliazimiwa pia wadau wadai nakala ya cheti cha kifo na sio kutaka cheti halisi na mengine. 

Sehemu ya Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke pamoja na Wadau wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (hayupo katika picha) alipokuwa akifungua Kikao cha wadau kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho.

Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka (katikati) akizungumza na Wadau hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho. Kushoto ni Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bw. Samson Mashalla na kulia ni Naibu Msajili Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Martha Mpaze.

 Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka akiendelea kuzungumza na Wadau (hawapo katika picha). Kulia ni Naibu Msajili Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Martha Mpaze.

Wadau wakimsikiliza Mhe. Mnyukwa (hayupo katika picha) wakati akifungua kikao hivi karibuni.

Wasilisho la Mada kuhusu Mirathi likitolewa na Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo-Temeke, Mhe Alois Mwageni wakati wa kikao kati ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke pamoja na Wadau wake. 

Wadau wakifuatilia mada ya Mirathi iliyokuwa ikitolewa na Mhe. Mwageni.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni