Jumanne, 22 Agosti 2023

JAJI LILA: JITOKEZENI KWA WINGI MAZOEZI YA BONANZA LA JMAT

 Na Magreth Kinabo-Mahakama

 JK kushiriki mazoezi leo na kesho


Mwenyekiti wa   Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Shabani Lila amewataka wanachama na watumishi wa Mahakama ya Tanzania kujitokeza kwa wingi katika mazoezi ya Bonanza maalum la michezo mbalimbali lililoandaliwa na JMAT mkoa wa Dar es Salaam ili liweze kutimiza malengo yake.

 

Akizungumza katika Viwanja vya Shule ya Sheria (Law School) vilivyopo jijini Dar es Salaam, jana tarehe 21, Agosti, 2023 Mhe. Jaji Lila ambaye ni Mwenyekiti wa Maandalizi wa Bonanza la JMAT Mkoa wa Dar es Salaam amesema  mazoezi ya michezo tofauti yanaendelea na tayari wameshafanya maandalizi ya kuwepo kwa vifaa vya michezo hiyo.

 

Aidha ameongeza kwamba  katika mazoezi hayo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani atashiriki leo tarehe 22, Agosti na kesho tarehe 23, 2023 kwenye viwanja hivyo, ni vyema ushiriki ukawa mkubwa katika mazoezi hayo.

 

Akizungumza kikao cha Viongozi wa JMAT wa Mkoa huo tarehe 10 Agosti, 2023 kwenye ukumbi wa maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Lila alisema lengo la Bonanza hilo ni kufahamiana, kuendeleza uhai wa chama hicho na kuamsha shughuli zake katika Mkoa huo.

 

“Tuna rasilimali kubwa katika chama tunaweza kufanya mambo makubwa, tukianza na Bonanza kwanza. Jambo linalotakiwa kufanywa sasa ni kuhamasisha wanachama ili waweze kushiriki,” alisema Jaji Lila, huku akisisitiza kwamba bonanza hilo litashirikisha familia za wanachama hao na kuwaalika watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa Mkoa huo.

 

Naye Katibu wa JMAT wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi ameitaja  baadhi ya michezo itakayochezwa katika Bonanza hilo ni mpira wa miguu na pete,kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na gunia, bao, draft, kukimbia mita 100 na mita 400 na kuendesha baiskeli mwendo wa polepole.

 

Kikao hicho kilishirikisha Viongozi wa matawi matatu ya JMAT kutoka, Mahakama ya Rufani Tanzania, Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu na Mahakama Kuu ya Ttanzania Kanda ya Dar es Salaam. 

 

Bonanza hilo limeandaliwa na JMAT Mkoa wa Dar es Salaam na litafanyika  tarehe 9 Septemba, 2023 kwenye viwanja hivyo.


Mwenyekiti wa   Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wa tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Shabani Lila (wa kwanza kulia)akizungumza jana tarehe 21, Agosti, 2023 kuhusu mazoezi hayo.

 





Picha za hapo juu ni baadhi wachezaji wa michezo mbalimbali wa Bonanza hilo wakiwa katika mazoezi ya viungo kwenye Viwanja vya Shule ya Sheria jana tarehe 21, Agosti, 2023. picha ya mwisho  kushoto wa kwanza ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Agnes Mgeyekwa.

Mwalimu wa Michezo, Waziri Mwemnao (mwenye jedi nyeusi)akiwaelekeza wachezaji kufanya mazoezi ya viungo, aliyevaa tisheti ya njano ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Gerson Mdemu, akifanya mazoezi na wachezaji hao.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Gerson Mdemu, akijiandaa kutoa pass katika mchezo wa mpira wa miguu.


Wachezaji wa mpira wa pete wakiwa katika mazoezi.

 


 

Picha  za juu ni  wachezaji wa mpira wa miguu wakiwa katika mazoezi.

                  Wachezaji wa mchezo wa kuvuta kamba wakiwa mazoezini.

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni