Na. Innocent Kansha, Sade Soka - Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ameuhakikishia
Uongozi wa Shule ya Sheria nchini kwamba, Mahakama ya Tanzania na Baraza la
Elimu ya Sheria “Council for Legal Education” kuendelea kutoa ushirikiano
katika jitihada za Taasisi hiyo ya kuboresha na kuandaa mtaala mpya utakao
kidhi matamanio ya wadau ili kuendana na mahitaji halisi ya taaluma ya sheria
katika karne ya 21.
Akizungumza
na Ujumbe wa Viongozi kutoka Shule ya Sheria nchini waliomtembelea Ofisini
kwake Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam leo tarehe 21 Agosti, 2023,
Jaji Kiongozi Mhe. Siyani amesema, shule ya sheria ndiyo chungu pekee cha kuwapikia wataalamu wa sheria
kwenye hatua ya mwisho kabisa katika sheria. Wahitimu wa shule ya
sheria ndiyo ambao wanaokuja kufanya kazi mahakamani wakiwa kama Mawakili ama
Mahakimu.
“Kwa
sasa jinsi sheria ilivyo hakuna hakimu ambaye tutamuajiri bila kupita na
kuhitimu shule ya sheria kwa vitendo kwani ni takwa la kisheria, kwa hiyo basi sisi
kama Mahakama tunashauku au matarajio makubwa na shule ya sheria kuona kwamba
wahitimu wanaozalishwa pale si tu kwamba wanakuwa na faida na jamii yetu pekee
lakini pia wanakuwa wako tayari kuja kuisaidia Mahakama kutimiza jukumu lake la
msingi la utoaji haki”, alisisitiza Mhe. Jaji Siyani.
Jaji
Kiongozi akaongeza kuwa, ndiyo maana mtaona na kutambua kuwa ukiondoa wajibu
ambao Mhe. Jaji Mkuu anao na akaukaimisha kwa Jaji Kiongozi wa kusimamia Baraza
la Elimu ya Sheria “CLE”. Kila wakati utaona Mahakama inavyojaribu kuwa karibu
na Shule ya Sheria, ziko taasisi na vyombo vingi vya Serikali vyenye wajibu na
Shule ya Sheria.
“Shule
ya Sheria naamini ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria hivyo basi Mahakama
ni wadau ambao tunajiweka karibu zaidi na Shule ya Sheria lakini mzazi wa kwanza
pale anapaswa kuwa wizara”.
Mhe.
Siyani akaongeza kuwa, “kwa kutambua nafasi yetu kwanza Kama Mahakama na pia
kama Baraza la Elimu ya Sheria ndiyo maana mnaona tunazidi kujiweka karibu
zaidi. Nafahamu kuhusiana na michakato mbalimbali inayoendelea ndani ya shule
ya sheria”.
Mahakama
itajaribu kujibu changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo kwa kipindi sasahivi,
kumekuwa na minong’ono kwamba watu wanasema kwa nini chakula kinachopikwa na
shule ya sheria hakiivi, wahitimu wengi wanaondoka wakiwa na manunguniko,
wengine wanafungua mashauri mahakamani lakini na wananchi kwa ujumla mpaka
ikapelekea mijadala mbalimbali.
“Sasa
nimefurahi kuona kwamba mtaala unaoandaliwa unaenda ungalau kujibu sehemu kubwa
ya changamoto ambazo zimekuwepo, hii ni hatua, naamini chuo kitaendelea
kutafakari na kuona namna gani ya kuboresha taaluma ili wahitimu wawe wenye
ubora na ufanisi katika utendaji kwa kutimiza ndoto na sababu za kuanzishwa
kwake ziwepo”, aliongeza Jaji Kiongozi
Mhe.
Siyani amesema, Kuanzishwa kwa Baraza la Shule ya Sheria katika miaka kadhaa iliyopita
sasa imekuwa ikifanya majukumu mengi zaidi ya kusimamia mitihani ya kutainiwa
kuwa mawakili wa kujitegemea, mitihani hiyo bado ipo ila ni kwa uchache sana
tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma mathalani mwaka jana tulisimamia watu
watatu (3). Kwa hiyo sehemu kubwa ya shughuli za Baraza ni kushughulikia
wanafunzi waliohitimu wanaotaka kuwa mawakili lazima watapita kwenye Baraza
Aidha,
Baraza hilo linatembelea kwenye Vyuo mbalimbali vinavyofundisha sheria na
kujadiliana kuona namna bora ya kuandaa wataalamu na kubadilishana mawazo kwa
lengo la kuboresha elimu ya sheria kuwa bora zaidi katika nchi yetu.
Jaji
Kiongozi aliongeza kuwa, Baraza linapokea mitaala na kuipitisha,
tumeshughulikia mitaala mingi ya vyuo mbalimbali ukiondoa Shule ya Sheria.
Baraza litaendelea na ziara ya kutembelea vyuo katika mikoa ya Kilimanjaro na
Arusha ifikapo mwezi wa Oktoba mwaka huu.
Jaji
Kiongozi akatolea ufafanuzi baadhi ya maombi yaliyotolewa na shule ya sheria ya
nafasi ya Baraza la Elimu ya Sheria kushughulikia kwa haraka mtaala huo mpya
utakapofika wa shule ya sheria. Baraza limewahakikishia shule ya sheria kuwa
linausubiri mtaala huo, watakapo umaliza na kuwasilishwa kwa Baraza. Baraza halitakuwa
kikwazo katika kuhakikisha kwamba shule ya sheria inatimiza kile walichokidhamiria
kwa kuwa na mtaala mpya utakaojibu changamoto nyingi zilizokuwepo.
“Sisi
tutakaa mara moja baada ya kupokea kutoka kwenu, kwa hiyo mkituletea mwezi wa
tisa tutatafuta nafasi yetu na Baraza kama nilivyosema halina Sekretarieti ya
kudumu tunategemea wataalamu wetu walewale ambao ni wajumbe kwa kuunda kamati
ndani yake ili wapewa andiko wasome baadae wanawasilisha mapendekezo mbele
ya Baraza tunajadiliana hatimaye tunapitisha,” alisema Jaji Kiongozi.
Akiwasilisha ujumbe kutoka Baraza la
Shule ya Sheria kwa Jaji Kiongozi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo,
Mhe. Clement Mashamba ambaye ni Kaimu Mkuu wa Shule Idara ya Mafunzo alitoa
pongezi na shukrani nyingi kwa Mahakama kuwawezesha kupata huduma za maeneo ya
kufanyia mikutano ya kukusanyia maoni ya kuboresha mtaala huo mpya katika
maeneo mbalimbali nchini takribani katika Masjala zote za Mahakama nchini
walikotembelea.
“Kamati
iliketi pale Mahakama Kuu Dodoma kwa takribani wiki mbili chini ya Mwenyekeiti
wetu Mhe. Dkt. Jaji Masabo tuliwezeshwa kutumia vifaa vya kisasa katika ukumbi
ule na tulifanya majukumu yet huku mahakama inaendelea bila mwingiliano wowote
na kwa utulivu wa kutosha naipongeza Mahakama kwa kuwa na miundombinu bora,”
aliongeza Mhe. Dkt. Mashamba
Mhe.
Dkt. Mashamba akasema jambo kubwa lililowafikisha Ofisini kwa Jaji Kiongozi ni kukuomba
kama Mwenyekiti wa Baraza la Shule ya Sheria na Mahakama inayoendelea kutupa
ushirikianao mkubwa, kwa mujibu wa sheria ya Mawakili na ya Shule ya Sheria shughuli
zote zinaendeshwa chini ya Baraza la Shule ya Sheria.
Kutokana
na mapendekezo ya Tume ya Mhe.Dkt. Mwakyembe ilihoji kwamba mtaala unaotumika
wa 2011 kama ulipelekwa katika Baraza la shule ya sheria ili upitishwe lakini
kutokana na hadidu rejea zilizopo hazikuonyesha nafasi ya Baraza la Shule ya
Sheria kushiriki kikamilifu katika mtaala uliopo.
“Tume
ikapendekeza kwamba katika mtaala unaoandaliwa ni sharti kamati ifanye kazi
bega kwa bega na Baraza la Shule ya Sheria, tunashukuru kwamba katika hatua
zote tumekuwa tukishirikiana na pia kamati iliundwa na mjumbe mmoja kutoka
Baraza la Shule ya Sheria na mwakilishi wa sekretarieti”, aliongeza Dkt.
Mashamba
Mhe.
Mashamba amesema mtaala huo mpya umeshakamilika kwa kupitia hatua zote ispokuwa
moja ambayo ni kuwaalika wadau wote wa nje kwa ajili ya kuupitia na kutoa mapendekezo
hatua itakayofanyika wiki hii na wakiridhia ndipo tutauwasilisha rasmi katika
Baraza la Shule ya Sheria kwa ajili ya baraka na kama kuna maelekezo zaidi ya
kitalamu. Kwa muongozo wa sheria ya shule ya sheria mtaala huo unapaswa kupewa
ithibati na Bodi ya shule ya sheria ambayo inatarajiwa kuketi tarehe 13 mwezi
Oktoba, 2023.
Hivyo
dhamira ya Bodi inakuomba kusaidia mchakato huu ukamilike mwaka huu ili
wanafunzi watakao dahiliwa mwakani waanze masomo yao kwa kutumia mtaala huo
mpya. Mtaala huo umeandaliwa kwa kuzingatia maeneo ya umahiri katika taaluma.
Pia mtaala huo unatolea ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwepo kwa zaidi ya asilimia
70.
Mhe.Dkt.
Mashamba akaiomba Mahakama kuendeleza ushirikiano wa kutoa wakufunzi wa
kufundisha kwani takribani asilimia 50 ya wakufunzi bado wanatoka Mahakama ya
Tanzania katika mafunzo ya hatua mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya sheria,
kwani mtaala mpya utategemea vitendo zaidi kuliko nadharia.
Pia
ujumbe huo ukaiomba Mahakama kuwapa kipaumbele wanafunzi wa shule ya sheria
wigo mpana wa kufanya mazoezi kwa vitendo ‘Field Attachment’ katika Mahakama
mbalimbali hapa nchini kwani mtaala mpya utamtaka mwanafunzi walau kufanya nusu
ya mazoezi yake yawe mahakamani ili kuwajengea uwezo mzuri na umahiri wa
kufanya kazi za kitaaluma na kuimarisha maadili ya kiwakili ambayo kwa sasa
yanamomonyoka sana, alisema Mhe. Dkt. Mashamba.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali wakati wa mkutano mfupi wakati alipotembelewa Ofisini kwake jijini Dar es Salaam na Ujumbe wa Viongozi kutoka Shule ya Sheria (hawapo pichana) mapema leo tarehe 21 Agosti, 2023 na kuuhakikishia Ujumbe huo kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu Shule ya Sheria nchini.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akisalimiana na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe mwelekezi na Mtaalamu wa kuuisha Mtaala Mpya wa Shule ya Sheria nchini, Mhe. Dkt. Fauz Twaib (kulia) mara walipokutana ofisini kwa Jaji Kiongozi jijini Dar es salaam mapema leo, wengine ni Wajumbe na Viongozi waandamizi wa Shule ya Sheria.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni