Jumatatu, 21 Agosti 2023

VIONGOZI MAHAKAMA MTWARA, LINDI WATEMBELEA UJENZI MAHAKAMA YA WILAYA LIWALE

Na Hilari Herman-Mahakama, Lindi

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Fredrick Lukuna, akiongozana na viongozi wengine waandamizi kutoka Kanda hiyo, hivi karibuni walitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama mpya ya Wilaya Liwale iliyopo katika Mkoa wa Lindi.

 Lengo la ukaguzi huo ilikuwa kubaini kama jengo hilo limekamilika bila kuacha dosari na kukudhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba au makubaliano kabla ya kukabidhiwa kwenye uongozi wa Mahakama.

Baada ya ukaguzi huo, Naibu Msajili na ujumbe wake walikaa kikao kuwapongeza Washauri, Wahandisi na Wakandarasi kwa kazi nzuri waliyofanya, kwani jengo la Mahakama hiyo limefikia  katika hatua za mwisho licha ya kasoro chache walizobaini ambazo walishauri zirekebishwe.

Kampuni ya Kiure Engineering Ltd inayojenga Mahakama hiyo imeahidi kurekebisha dosari chache zilizobainishwa wakati wa ukaguzi huo kabla ya kukabidhi jengo hilo ifikapo tarehe 16 Septemba, 2023.

Baada ya shughuli hiyo ya ukaguzi, Viongozi wa Mahakama Kanda ya Mtwara walipata wasaa wa kuzungumza machache na watumishi wa Mahakma ya Wilaya ya Liwale, huku Mhe. Lukuna akiwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hata hivyo, aliwataka kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha aliwasisitiza watumishi hao kuendelea kutoa huduma iliyo bora na ya kuridhisha kwa wadau wa Mahakama na wananchi kwa ujumla.

Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Liwale (mbele na nyuma).

Mkadiliaji Majenzi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Deogratias Lukansola akifafanua jambo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni