Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Wanafunzi wa
Darasa la Saba Shule ya Msingi Mwagala iliyopo Manispaa ya Shinyanga wamepata
nafasi ya kujifunza muundo wa Mahakama ya Tanzania na utendaji kazi wa Mhimili
huo wenye jukumu la kutoa haki nchini, hivyo kuwa na ndoto ya kuwa Majaji na
Mahakimu watakapohitimu masomo yao.
Wanafunzi hao wanaotarajia
kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi mwezi Septemba mwaka huu, wakiongozwa
na Mwalimu wa Somo la Uraia na Maadili, Mwl. Peter Daniel, walifika katika
jengo la Mahakama Kuu Shinyanga hivi karibuni na kukutana na Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga Mhe. Seif Kulita.
Mhe. Kulita
aliwafundisha muundo wa Mahakama na jinsi unavyofanya kazi kuanzia Mahakama ya
Rufani hadi Mahakama ya Mwanzo. Jaji Kulita alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania
inalo jukumu la kutoa haki nchini na maamuzi yanayotolewa hayaingiliwi na mtu
yoyote kwa sababu ndiyo chombo pekee kilichopewa mamlaka hayo kikatiba.
Wanafunzi hao walifurahi
kupata maelezo hayo na kuonyesha shauku ya kuwa Majaji na Mahakimu hapo baadaye
watakapomaliza masomo yao na kuahidi kusoma kwa bidii kufikia ndoto hiyo ili na
wao siku moja waje kutekeleza jukumu la kutoa haki.
Awali, akifundisha
juu ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania (2020/2021–2024/2025),
Hakimu Mkazi, Mhe. Dushi Peter aliwaeleza wanafunzi hao namna Mahakama ya
Tanzania inavyoendelea kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha
utendaji kazi wa kila siku ili kuendana na dhana nzima ya utoaji haki kwa
wananchi na kwa wakati.
Alieleza mafanikio
ambayo Mahakama ya Tanzania imeyapata hadi sasa, ikiwemo uimarishwaji wa mifumo
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji
Haki nchini na Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.
Aidha, alieleza
kuhusu kuimarika kwa huduma za kimahakama, ikiwemo utoaji nakala za hukumu kwa
wananchi siku ambayo shauri lake litamalizika Mahakamani.
Wanafunzi hao walionyesha
kufurahi zaidi walipotembelea Mahakama ya wazi, kujibu maswali mbalimbali ya
kimahakama na kuahidi wako tayari kuukabili vyema mtihani wa Somo la Uraia na
Maadili hapo Septemba, 2023.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Dushi
Peter akitoa mada kuhusu Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa wanafunzi
hao.
Mwalimu wa Somo la Uraia na Maadili Shule ya Msingi Mwagala Peter Daniel akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwagala.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwagala
wakiwa wamenyoosha mikono juu kuashiria kuwa na ndoto ya kuwa Majaji baada ya
kuulizwa iwapo wanandoto hiyo.
Mwanafunzi Moris Zacharia akitoa shukrani
kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita
(hayupo katika picha) baada ya kupata elimu ya muundo wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Mhe. Seif Kulita akiwa katika mpicha ya pamoja na wanafunzi wa Shule
ya Msingi Mwagala walipofika mofisini kwake kujifunza Muundo wa Mahakama ya
Tanzania.
Picha ya pamoja ya wanafunzi wa Shule ya
Msingi Mwagala walipotembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni