Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma
Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Kigoma hivi karibuni walitembelea Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe,
Mhe. Col. Michael Ngayalina, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa nguzo ya tatu ya
Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021–2024/2025) inayosisitiza kuimarisha
ushirikiano na wadau.
Ujumbe huo wa Mahakama
uliongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe.
Lameck Mlacha akiwa ameambatana na Jaji mwenzake wa Mahakama Kuu, Mhe. Stephen
Magoiga na wenyeji wao, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe.
Katoki Mwakitalu na Katibu Tawala wa Wilaya, Bi. Utefta Mahega.
Baada ya kupokea ugeni
huo, Mkuu wa Wilaya alifurahishwa kwa ujio wa Majaji hao kwenda kumtembelea
ofisini kwake kwa nia ya kukuza mahusiano ya kitaasisi katika Mkoa wa Kigoma.
Aliwaeleza viongozi hao
kuwa Wilaya yake ni salama na hali ya hewa ni nzuri, ina chakula cha kutosha. Mhe.
Col. Ngayalina aliwaomba, kama wakipata muda mwingine, watembelee maeneo
mbalimbali ya Wilaya hiyo ili kujionea uzuri na mandhari yake.
Majaji walifurahishwa na Uongozi
huo wa Wilaya kwa mapokezi na kuwapongeza kwa jengo zuri na la kisasa ambalo
limechukua idara mbalimbali zinazotoa huduma kwa wananchi katika Wilaya hiyo.
Majaji hao walikuwa
katika ziara ya kimahakama kwenye Wilaya hiyo kwa lengo la kuwakutanisha pamoja
watumishi katika michezo.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Col. Michael Ngayalina (katikati) akifurahia jambo baada ya kuwapokea wageni wake, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma.
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni