·Atembelea pia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Na.
Faustine Kapama-Mahakama
Ziara ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija na ujumbe wake imeingia siku ya nne leo tarehe
18 Agosti, 2023 ambapo ametembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,
ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ambayo alipatia Shahada ya Udakitari wa Sheria.
Maeneo mengine aliyotembelea ni Posta kwenye
mzunguko wa Askali Monament, Makumbusho ya Taifa pamoja na Kijiji cha
Makumbusho kilichopo Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni.
Ziara yake ilianza kwa kutembelea kwenye
mzunguko wa Askali Monament na kupata
maelezo mafupi kutoka kwa wenyenji wake, akiwemo Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt na Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Bi.
Mary Shirima, kabla ya kuelekea Makumbusho ya Taifa.
Akiwa katika Makumbusho hayo, Mhe. Dkt. Zaija ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Dk. Pius Biligimana alijionea historia mbalimbali zilizohifadhiwa katika eneo hilo, ikiwemo magari aliyowahi kuyatumia Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambalage Nyerere wakati wa uongozi wake.
Baadaye Jaji Kiongozi wa Uganda alielekea
katika Kijiji cha Makumbusho Kijitonyana na kujionea nyumba za makabila
mbalimbali kabla ya kupata burudani kutoka kwenye Kikundi cha Ngoma cha Mpolo
Dancing Troupe.
Akiwa katika Kijiji hicho, Mhe. Dkt. Zeija
alielezea kufurahishwa na hifadhi hiyo ambayo ni kumbukumbu muhimu kwa vizazi vya
sasa na vijavyo. Amesema kumbukumbu iliyohifadhiwa katika Kijiji hicho inatoa
fundisho kubwa kuwa Afrika ni moja na jinsi mababu zetu walivyokuwa na welevu
wa kutosha katika kuimarisha ustawi katika jamii.
“Kwa kuangalia Kijiji hiki inaonyesha tu
kwamba sisi ni wamoja. Lakini pia kinaonyesha umuhimu wa kuhifadhi utamaduni.
Hii ni kwa sababu watoto wetu wanaweza kuwa hawakuishi kuishi katika nyumba hizi
na wasingejua. Lakini tunapokuwa na hifadhi kama hizi watoto wetu watajua jinsi
mababu zao walivyokuwa wanaishi,” amesema.
Baadaye, Jaji Kiongozi wa Uganda na jumbe
wake alielekea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupokelewa na Kaimu Mkuu
wa Chuo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masomo ya Uzamili, Prof. Donatha Tibuhwa na
baadaye kukutana na Mwalimu wake, Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo hicho, Dkt.
Sosithenes Materu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni