Na Aidan Robert- Mahakama, Kigoma
Mkurugenzi Idara ya Huduma za Uangalizi Taifa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Aloyce Musika ameipongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, kwa maboresho makubwa yanayogusa maisha ya wananchi na Watumishi hasa katika kuhabarisha umma juu ya kila jambo linalo endelea Mahakamani.
Akizungumza hivi karibuni wakati alipowatambulisha maafisa wapya ambao watafanya shughuli zao za kutoa huduma za uangalizi kwa washitakiwa wanaopewa adhabu mubadala zitolewazo na Mahakama ya Tanzania mkoani Kigoma, alisema ameshuhudia Mahakama za kisasa zenye miundombinu mizuri na rafiki kwa watumishi katika kuharakisha utoaji haki kwa wananchi.
“Nimefurahishwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi kuwa katika jengo la kisasa la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, na huu ni udhihirisho kwamba haki inapatikana kwa wakati bila kutumia gharama, alisema Musika.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kigoma, Mhe. Rose ameishukuru ofisi hiyo kwa kuendelea kuongeza nguvu kazi kwa kuwa ni maafisa wawili pekee ndio wanaotoa huduma mkoani hapa. ambao watafanya shughuli zao za kutoa huduma ya uangalizi kwa washitakiwa wanaopewa adhabu mubadala zitolewazo na Mahakama ya Tanzania mkoani Kigoma.
Alisema maafisa hao walilazimika kutoa huduma hiyo katika Mahakama zote za Mkoa huo, hivyo walioongezeka wataongeza nguvu ya kuisaidia Mahakama katika kutekeleza adhabu mbadala zitolewazo kwa washitakiwa.
Maafisa waliotambulishwa ni Bw. Kelvin Kulaya, na Bw. Ramadhan Ramadhan, ambapo Mhe. Rose amewataka kufanya kazi kwa weledi, kujituma, maana Kigoma ni sehemu nzuri ya kufanyia kazi.
Akimshukuru Hakimu Mkazi, Afisa Huduma za Uangalizi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma Bw. Samwel Kabunga, alisema anaishukuru Mahakama hiyo kwa ushirikiano anaoupata hasa wanapotekeleza majukumu yao mahakamani.
Mkurugenzi wa Huduma za Uangalizi Taifa, Bw. Aloyce Musika, akisisitiza jambo alipokuwa akitoa maelezo ya kuwatambulisha maafisa wapya wa ofisi hiyo.
Bw. Kelvin Kulaya, Afisa mwajiliwa mpya katika Ofisi ya Idara ya Huduma za Uangalizi Mkoa wa Kigoma, akisikiliza kwa makini maelekezo ya Mkurugenzi huyo.
Bw. Ramadhan Abdul Ramadhan, Afisa mwajiliwa mpya katika Ofisi ya Idara ya Huduma za Uangalizi Mkoa wa Kigoma, akiwa makini kusikiliza maelekezo toka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni