Ijumaa, 18 Agosti 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA NJOMBE WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Na Abdallah Salum-Mahakama, Njombe

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe wamehimizwa kufanya kazi kwa weledi na kuelewa kwa ufasaha dira ya Mahakama katika muktadha mzima wa utoaji wa huduma za haki zinayomlenga mwananchi.

Wito huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama hivi karibuni alipokuwa anazungumza na watumishi hao kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa wazi katika Mahakama hiyo.

Mhe. Chamshama alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kujua nguzo zote tatu katika Mapango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama (2020/2021- 2024/25) zinazolenga kwenye utoaji wa haki kwa wakati.

“Itakuwa maajabu kwa mtumishi wa Mahakama kutojua Dira ya Mahakama kwa nyakati kama hizi za sasa, ambapo Mahakama inafanya maboresho makubwa kupitia mikakati hiliyojiangia,” alisema, huku akiwahimiza watumishi wote kufanya kazi kubaguana kidini, kikabila au kijinsia bali watekeleze majuku yao wakiwa wamoja.

Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi pia alisisitiza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye ofisi zao kwani imekuwa ikirahisisha kazi za kimahakama, hasa kwenye kupata takwimu kiurahisi na kwa njia ya haraka.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Njombe, Bw. Yusuph Msawanga alisisitiza muhimu wa utoaji wa elimu na mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi na jamii kutoka taasisi zingine kwa kushirikiana na kamati ya elimu ya Mkoa kwenye masuala mbalimbali ili kumsaidia mwananchi kupata haki.


 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama akiongea na watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe.

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Njombe, Bw. Yusuph Msawanga akisisitiza jambo katika kikao hicho.

Sehemu ya watumishi wakiwa katika kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni