Ijumaa, 18 Agosti 2023

JAJI MFAWIDHI SUMBAWANGA ATAKA WANASIASA KUHESHIMU AMRI ZA MAHAKAMA

Na Mayanga Someke – Mahakama Kuu, Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma ameiomba Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoa ushauri na maelekezo kwa Viongozi wa siasa kuheshimu amri za Mahakama.

Mhe. Mruma alitoa wito huo hivi karibuni alipotembelewa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo na kusisitiza kuwa Viongozi hao wa siasa wanatakiwa kuacha kuingilia utekelezaji wa amri za Mahakama zinazotolewa.

“Niwaombe Mawakili wa Serikali kutoa ushauri na maelekezo kwa viongozi wa kisiasa waweze kuheshimu amri za Mahakama,” alisema. Jaji Mfawidhi alitumia nafasi hiyo kuwahimiza Mawakili hao kufanya maandalizi ya kutosha katika uendeshaji wa mashauri ya madai mahakamani.

“Naomba muwe wakweli ili kuisaidia Mahakama kutenda haki na kuishauri vema Serikali ili kuepusha gharama zisizo za lazima,” Mhe. Mruma alisisitiza.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa suala la kubadilisha mara kwa mara Mawakili katika kesi za Serikali linasababisha maombi ya kuahirisha usikilizaji, hivyo kuchangia ucheleweshaji.

Amewashauri pia Mawakili wa Serikali kutumia taarifa za mashahidi (witness statement) wakati wa usikizaji wa mashauri na kuanza majadiliano na usuluhishi kabla ya kuja mahakamani.

Katika mazungumzo yake na Jaji Mfawidhi, Bi. Mwaipopo alimweleza dhumuni la ujio wake, ambalo ni kujionea utendaji wa shughuli za ofisi yao na kuhimiza ushirikiano wa pamoja na wadau, ikiwemo Mahakama.

“Nipo katika ziara ya kikazi ya kuangalia utekelezaji katika ofisi zetu za Mikoa na imenibidi nije kuonana na kushauriana namna ya kuyamaliza mashauri yaliyopo mahakamani na katika Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya,” alieleza.

Naibu Wakili Mkuu alibainisha kuwa kuna jumla ya mashauri 27 kwa Kanda ya Sumbawanga ambapo kati ya hayo, mashauri 10 yako Mahakama Kuu na yaliyobaki yapo kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya Sumbawanga na Mpanda.

“Nitakaa na Wanasheria wa Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ili kutoa maelekezo juu ya uendeshaji wa kesi zinazohusu Serikali. Pia kuwapitisha Mawakili wa Serikali katika mabadiliko ya Sheria, ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (Civil Procedure Code),” alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma akieleza jambo.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi.Sara Duncan Mwaipopo akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amir Mruma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma akiwa na mgeni wake, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sara Mwaipopo (wa kwanza kulia waliokaa mstari wa juu). Wengine katika picha ni Naibu Msajii wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Maira Kasonde (wa kwanza kulia waliokaa mstari wa chini) pamoja na wageni wengine.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma kitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya ugeni uliomtembelea ofisini kwake.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni