Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama
Jaji wa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania, Mhe. Omar Makungu ameapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Haki
ya Afrika Mashariki, Divisheni ya Rufani.
Rais wa Burundi, ambaye
ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Évariste
Ndayishimiye aliongoza hafla ya uapisho huo tarehe 22 Agosti, 2023 katika
sherehe iliyofanyika Ikulu ya Ntare, Bujumbura, nchini Burundi.
Kwa mujibu wa tovuti ya
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, kiapo cha Jaji huyo mpya kilitolewa na
Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Christine Mutimura, akisaidiwa na Wakili
wa Jumuiya hiyo, Dkt. Anthony Kafumbe.
Jaji Makungu, ambaye kwa
sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, anachukua nafasi ya aliyekuwa Jaji
katika Mahakama hiyo, Mhe. Sauda Mjasiri, ambaye amefikisha umri wake wa
kustaafu.
Baada ya uapisho huo, Mwenyekiti
wa Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alimpongeza Jaji Makungu na
kumtakia kheri katika kazi zake za kimahakama.
Hafla ya uapisho huo ilihudhuriwa
na viongozi mbalimbali, akiwemo Ofisa Mkuu Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi, Salvator
Mbilinyi.
Wengine ni Waziri wa
Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Burundi, Domine Banyankimbona, Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera na Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Severin Mbarubukeye.
Mhe. Makungu aliteuliwa
kushika wadhifa huo katika Mkutano wa Marais wa Nchi Wanachama wa Afrika
Mashariki uliofanyika Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei, 2023.
Mkutano huo ulifanyika
kujadili mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usalama Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC).
Katika mkutano huo,
kulifanyika pia uteuzi wa Majaji wengine, Mhe. Anita Mugeni kutoka Rwanda
anayekuwa Makamu Rais wa Mahakama hiyo na Mhe. Kayembe Rene kutoka DRC ambaye
anakuwa Jaji wa Mahakama katika Divisheni ya Awali.
Mhe. Makungu amewahi kuwa
Jaji Mkuu wa Zanzibar kabla ya kuteliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni