Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha hivi karibuni aliongoza
kikao cha Kamati ya Uongozi Kanda ya Kigoma kutathimini utendaji kazi na kuweka
mikakati ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama.
Kikao hicho kilichohudhuriwa
na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga na
wajumbe wengine kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mahakama za Wilaya
Kigoma, Kibondo, Kasulu, Uvinza, Kakonko na Buhigwe kilifanyika katika ukumbi
wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe.
Akizungumza wakati
anafungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwataka wajumbe kuendelea kusimamia na
kutekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa na Viongozi wa Mahakama kupitia waraka
wa Jaji Mkuu 1/2023 na Waraka wa Jaji Kiongozi Na. 3/2019.
Nyaraka hizo zinahusu utoaji
wa nakalau za hukumu na kuchapa mienendo ya mashauri ndani ya siku 14 na utumaji
wa majalada yanayoitishwa na Mahakama za juu ndani ya siku 21.
Katika kikao hicho, Mhe.
Mlacha aliushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa namna ulivyoutafsiri kwa
vitendo Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021–2024/2025) Kanda ya Kigoma kwa
kuongeza na kujenga majengo mapya matatu, kununua magari manne na kuleta
watumishi wapya 11 wa kada mbalimbali, hatua itakayowezesha utekelezaji wa dira
ya Mahakama ya Utoaji wa Haki kwa wakati.
“Tumepata majengo mapya,
vyombo vya usafiri na waajiriwa wapya. Tunapaswa kuyatunza majengo haya na
vyombo vya usafiri na kuwalea vyema waajiriwa hawa wapya,” alisema.
Wajumbe wa kikao walipata fursa pia ya kupata mafunzo jinsi ya kushughulikia malalamiko kimtandao (e-Complaints) yaliyotolewa na Afisa TEHAMA, Bw. Prosper Mahalala.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akisisitiza jambo wakati
wa kikao kazi cha Viongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma.
Jaji wa Mahakama Kuu
Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga akitia saini katika kitabu cha wageni katika ofisi
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Buhigwe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akisalimiana na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Mkoa wa Kigoma.
Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga akisalimiana na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Mkoa wa Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni