Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messeka Chaba leo tarehe 24 Agosti, 2023
ameendesha kikao cha maandalizi ya awali ya vikao vya kusikiliza mashauri ya mauaji.
Kikao hicho kilichofanyika
katika Ukumbi wa Mkutano ulipo katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
Morogoro kiliwajumuisha wadau mbalimbali wa wa haki jinai ambao ni wahusika
katika kesi zitakazosikilizwa. Walikuwepo pia viongozi upande wa utawala,
akiwemo Mtendaji wa Mahakama Seleman Ng’eni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa kikao hicho, Mhe. Chaba alisema wamekutana kuweka mikakati ya pamoja ya
kufanikisha usikilizwaji wa mashauri, ikiwemo kujua kama kuna mapungufu yeyote ili
yaweze kurekebishwa mapema.
Aliwaomba wadau wote kutoa
ushirikiano na mchango wao wa mawazo kuwezesha mashauri yote kusikilizwa ndani
ya muda uliopangwa. Alisisitiza kuwa ikitokea changamoto yeyote wakati vikao
vinaendelea wasisite kuitolea taarifa ili iweze kutatuliwa mapema.
“Natambua kuwa sisi wote ni
binadamu, wakati mwingine kuna dharura zinajitokeza, hivyo msisite kutoa
taarifa mapema na haitachukuliwa kama mwanya wa kukwamisha vikao hivi,” Mhe.
Chaba alisisitiza na kutoa shukurani kwa ushirikiano anaoupata toka kwa wadau
hao.
Awali, wakati akisoma taarifa
ya kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Augustina
Mmbando alisema kuwa jumla ya mashauri 12 yamepangwa kusikilizwa kwenye kikao
kitakachoanza tarehe 28 Agosti hadi tarehe 29 Septemba, 2023 mbele ya Mhe.
Chaba.
Alisema kuwa kati ya mashauri
hayo, 11 yanahusu mauaji ya kukusudia na shauri moja ni la mauaji ya
kutokukusudia. “Ni matarajio yetu kupitia kikao hiki sote tutashiriki
kuhakikisha mashauri yote 12 yaliyopangwa yanasikilizwa na kumalizika kwa
wakati. Niwaombe wote tufike mahakamani kwa wakati,’’ alisema.
Kikao kingine kitakuwa chini
ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Paul Ngwembe ambaye
anatarajia kusikiliza mashauri 11 huko wilayani Kilombero.
Naye Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka
Kanda ya Morogoro, Bi. Neema Haule alisema kuwa ofisi yake imejipanga vizuri,
wameyasoma majalada ya mashauri hayo vizuri na wamejiandaa kuleta mashahidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni