Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha ametoa wito kwa watumishi
wote wa Mahakama mkoani Kigoma kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ili
kuimarisha afya na kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Mhe. Mlacha alitoa wito
huo hivi karibuni kwenye Bonanza lililokutanisha pamoja timu ya watumishi wa
Mahakama mkoani Kigoma na timu ya mpira wa miguu kwa watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya Buhigwe.
“Niwaombe Waratibu wa
vikao vijavyo mtuandalia michezo tukikutana ili kuimarisha afya na mahusiano
baina ya taasisi” alisema.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu
Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga, aliwajulisha washiriki wa Bonanza hilo kujenga
utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Alibainisha kuwa yeye
pamoja na Jaji Mfawidhi kila siku alfajiri wanafanya mazoezi kwa kutembea
wastani wa kilomita tano kwenye vilima, hivyo ni vizuri kuiga mfano huo.
Kwa upande wake, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe Gadiel Mariki, ambaye alikuwa
sehemu ya wachezaji wa timu ya Mahakama hiyo alijizolea umaarufu baada ya
mashabiki kumpachika jina la mchezaji maarufu wa timu ya Yanga ‘Skudu’ kutokana
na aina ya uchezaji wake.
Mtanange huo uliokuwa wa
vuta ni kuvute uliisha kwa Mahakama Kigoma kupoteza mchezo huo kwa idadi ya
magoli mawili kwa nunge. Wachezaji wamemuahidi
Jaji Mfawidhi kuwa watasahihisha makosa madogo yaliyotokea ili kuchagiza
ushindi katika mechi zijazo, kwani mchezo huo umekuwa funzo kwao.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Katoki Mwakitalu, aliishukulu timu pinzani kwa kukubali
kushiriki kwenye mchezo huo ambao ni sehemu ya kukuza mahusiano mema na wadau
katika Wilaya hiyo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akifuatilia pamoja na Jaji Stephen Magoiga na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Rose Kangwa, mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu kati ya Timu ya Mahakama na Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe katika uwanja wa Shule ya Msingi Buhigwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni