·Waacha alama ya kutukuka mahakamani
·Kasi ya Jaji Makani kuamua mashauri mfano wa kuigwa
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani leo tarehe 31 Agosti, 2023
ameongoza Majaji na watumishi wa Mahakama kuwaaga kitaaluma Majaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Moses Mzuna na Mhe. Victoria Makani, ambao wamestaafu katika
utumishi wa umma.
Hafla ya kuwaaga Majaji hao
imefanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Divisheni, Bi. Mary Shirima, Naibu Wasajili, Watendaji, ndugu na jamaa wa
wastaafu hao.
Zoezi la kuwaaga viongozi
hao lilianza kwa mashauri mawili Namba 2, 2023 na Namba 3, 2023 yaliyokuwa yanawahusu
Mhe. Mzuna na Mhe. Makani, mtawalia, kuunganishwa pamoja kabla ya kuruhusu
Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chama cha Mawakili Tanganyika
(TLS) kuwasilisha hoja zao.
Akiwasilisha hoja zake,
Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Camilius Ruhinda alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 33 ambacho Jaji Mzuna amefanya
kazi akiwa Hakimu, Msajili na baadae Jaji, aliweza kutoa maamuzi mbalimbali
ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika jukumu la utoaji haki nchini.
“Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mhe. Mzuna katika kutenda haki kupitia
maisha yake ambayo yanadhihirika hususan katika hukumu mbalimbali alizowahi
kutoa. Ni wazi kuwa hatuwezi kuandika mambo mengi kwa kuwa wasaa hautoshi; ila
inatosha kusema kuwa tumefanya naye kazi na tutaendelea kuenzi maisha yake
katika kutetea haki ambayo ni msingi mkuu katika utekelezaji wa sheria,”
alisema.
Kwa upande wa Mhe. Makani, Wakili wa Serikali alisema
kuwa katika utumishi wake akiwa Jaji aliweza kutoa maamuzi mbalimbali ambayo
yalionyesha umuhimu wa kufuata sheria katika kutatua migogoro. Alisema kuwa
maamuzi mengi aliyotoa yanahimiza kuwa makini katika kufuata utaratibu
uliowekwa kisheria ili haki iweze kutendeka.
“Tunakupongeza kwa kusimamia
sheria na kutoa maamuzi ambayo kwa nafasi kubwa tumeendelea kuyatumia katika mashauri
mengine. Tutaendelea kujifunza kutoka kwako hususan usimamiaji wa sheria. Ofisi
ya Wakili Mkuu wa Serikali inakutakia heri na baraka katika maisha yako,”
alisema.
Makamu Rais wa TLS, Bi.
Aisha Sinda, akiwasilisha hoja kwa niaba ya Rais wa Chama hicho, alieleza kuwa moja
ya kigezo kikubwa katika upatikanaji wa haki ni uwepo wa watendaji mahiri
katika Mahakama, hasa Majaji.
Alisema TLS inafarijika pale
ambapo wanachama wao ambao pia ni maafisa wa Mahakama, wanapofanya kazi na Mhimili
ambao unaundwa na watendaji waadilifu, wanaosimamia misingi ya haki pasipo
kuyumbishwa na wenye kujali taratibu za kazi kama ilivyokua kwa Majaji Mzuna na
Makani.
“Kwa niaba ya baraza la
uongozi wa TLS tunawakaribisha sana Majaji hawa wastaafu tena katika chama
chetu cha wanasheria, imekuwa ni kawaida sasa kwa Majaji wastaafu kurejea
kufanya shughuli za uwakili. Tunapenda kuwafahamisha kuwa chama kitakuwa tayari
kuwapa ushirikiano wa kutosha katika ngazi zote,” alisema.
Baada ya hoja hizo kuwasilishwa,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Mhe. Latifa Mansoor,
alimwelezea Mhe. Mzuna kuwa amefanya
kazi nzuri katika Mahakama ya Tanzania na kuchangia katika utawala wa haki kwa
ujumla, hali ambayo ilijidhihirisha mara kadhaa wakati wa kuamua mashauri
mbalimbali yaliyoletwa mbele yake.
Alieleza kuwa katika utawala wa haki, Jaji Mzuna alikuwa imara katika
kusimamia sheria na haki ambapo haki ilionekana inatendeka ipasavyo kwa kuwa
aliheshimu na kuzingatia misingi ya haki asilia.
Mhe. Mansoor alisema hukumu zilizotolewa na Jaji Mzuna ziliamuliwa bila
upendeleo, zilizingatia hoja nzuri na msingi zilizopelekea mashauri kuamriwa
kwa wakati na katika jukumu la kutenda haki alikuwa anajali makundi yenye
mahitaji maalum, wakiwemo wajane.
“Tutamkumbuka sana Jaji Mzuna kutokana na mchango wake katika maisha ya kitaaluma na
ya ushiriki wake katika kudumisha utamaduni wa
Mahakama ya Tanzania. Yeye ni mmoja wa waliojitoa kwa kazi yao na kuhakikisha kuwa haki
inatolewa kwa wakati,” alisema.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda alimwelezea Jaji Makani kama
mtumishi wa umma aliyetekeleza majukumu yake kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa,
ikiwemo kusikiliza mashauri na kutoa maamuzi kwa wakati.
“Takwimu zinaonesha kwamba kwa kipindi chote cha
kuanzia mwaka 2019 Mei hadi siku yake ya mwisho ya utumishi wa umma tarehe 4
Mei, 2023, ikiwa ni muda ambao alitumikia Divisheni ya Ardhi, Jaji Makani aliweza
kusikiliza na kuamua jumla ya mashauri 861,” alisema.
Mhe.
Luvanda alieleza kupata nafasi ya kuongea na watumishi waliofanya kazi na Jaji Makani
ambapo Majaji wameonesha kuwa kuondoka kwake imekuwa haraka ukilinganisha na
uwezo au umahiri wake.
“Wengi
wametamani angebaki kwa muda zaidi ili aendelee kuandaa maandiko muhimu kwa
mashauri yanayoendelea kufunguliwa, kwani kwa mashauri aliyosikiliza
alifanikiwa kuonesha umahiri mkubwa na msimamo chanya zaidi kulingana na matakwa
ya kisheria,” alisema.
Baada
ya maelezo hayo, Jaji Kiongozi alitoa amri kadhaa za kuhitimisha mashauri hayo
na kuwashukuru wote waliohudhuria hafla hiyo ya kitaaluma ya kuwaaga Majaji hao
wa Mahakama Kuu, ambao wamestaafu rasmi katika utumishi wa umma.
“Kwa niaba yangu na kwa niaba ya (Majaji
wengine wa Mahakama Kuu) ambao kwa pamoja tumesikiliza mwenendo wa mashauri haya
maalumu ya kuenzi kazi za kitaaluma, sasa natamka kuwa Majaji Wastaafu, Mhe.
Moses Mzuna na Mhe. Victoria Makani wameagwa kitaaluma na kwamba wamestaafu
rasmi utumishi wa umma,” amesema.
Jaji Mzuna alianza safari yake ya utumishi katika Mahakama ya Tanzania tarehe 31 Machi, 1990 alipoajiriwa kama Hakimu
Mkazi. Amehudumu katika nyadhifa mbalimbali kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 26 Juni, 2009.
Kwa upande wake, Jaji Makani amehudumu katika nafasi
mbalimbali katika fani ya sheria kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania mwaka 2015.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni