Ijumaa, 1 Septemba 2023

JAJI MZUNA NA VICTORIA WASIMULIA WALIYOJIFUNZA


Magreth Kinabo-Mahakama na Sade Soka(UDSM)

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Moses Mzuna amesema kuna mambo mengi aliyojifunza katika jukumu lake la utaoaji haki nchini, likiwemo la uvumilivu na kutoa uamuzi sio kwa kuangali sheria., bali hata kutumia nguvu ya ushawishi na ushirikiano, huku Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Mhe. Victoria Makani amesema jukumu hilo linahitaji jicho la pili linalopatikana kwa Mungu.

Aidha Mhe. Jaji Mzuna amewasihi Wahe. Majaji ambao amewaachia kijiti  kuendelea kutekeleza wajibu wao  ambao Mwenyezi Mungu amewakabidhi katika kutenda  haki kwa, uaminifu, uadilifu na kwa weledi mkubwa, kuzingatia misingi na miiko ya taaluma  hiyo na  ushirikiano mkubwa  ili kuendelea kuenda sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano wa mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.

Hafla ya kuwaaga huyo na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Mhe. Victoria Makani iliyofanyika Agosti 31,2023 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliopo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni, Bi. Mary Shirima, Naibu Wasajili, Watendaji, ndugu na jamaa wa wastaafu hao.

 

Mhe.Jaji Mzuna  amesema amejifunza hayo  kupitia tukio alilolikumbuka wakati  alipokuwa Mwanza, mwaka wake  wa kwanza wa utendaji kazi wake, akiwa na umri wa miaka 27.

 

“Nilipangiwa kesi ya ndoa “matrimonial” ambapo Baba mwenye umri kama miaka 70 alitaka kumpa talaka mke wake wa miaka kama 65. Baada ya kulisoma jalada niliwaita. Walipoingia ndani niliwaeleza kuwa wao ni sawa na Baba na Mama yangu, hivi kweli wanataka mimi mtoto wao nitoe talaka? Walikuwa tayari wametengana takribani miaka miwili.  Baba akawaza mara mbili. Kuna jambo walinong’onezana. Nikawaambia nawapa muda wa siku mbili waende, watafakari halafu warudi ili tuanze kulisikiliza shauri hilo kama kweli wameamua hivyo,” amesema.

 

Alifafanua kuwa baada ya siku mbili, walirudi wakamwambia kuwa wamesharudiana na wanaishi pamoja. Hakuna haja ya talaka tena. Shauri hilo likaondolewa kwa makubalianao yao ya bila masharti yoyote. “Hapo nikaona kumbe uamuzi siyo lazima kutumia nguvu ya sheria bali ushawishi pia ni jibu. Tukumbuke miaka hiyo suala la usuluhishi kisheria “mediation” lilikuwa halijaanza. Ni ubunifu tu na nguvu ya ushawishi kutokana na mazingira unayoyaona,”.

Hivyo katika utumishi wao wanakutana na mambo mengi, mazuri na mabaya. Kitu cha muhimu wanapaswa kufanya kazi zao kwa uvumilivu, uadilifu na kujituma. kumuweke Mungu mbele kwa kuwa wananchi na wadaawa wana kitu kizuri cha faraja cha kuwakumbuka.

“Tuwe waangalifu katika kazi yetu ya kutenda haki, tuwe na uvumilivu, uadilifu, kumwomba Mwenyezi Mungu, kutochagua kazi au kituo cha kufanyia kazi.Tuendeleze ushirikiano na wadau wengine wa haki ili kuhakikisha kuwa dira ya mahakama na mipango yake ya maendeleo kuelekea mapinduzi ya kiteknolojia inafikiwa na inakuwa endelevu,” amesema Mhe. Jaji Mzuna wakati akitoa hotuba yake ya kusaafu.

Ameongeza kwamba kwa karne ya sasa ni muhimu kushirikiana na mihimili mingine ya Serikali ili kuendelea kuongeza imani kwa umma ambayo Mahakama imejitolea kuitumikia.

“Nafurahi kuwa nastaafu wakati ambao Mahakama ikiwa na sifa nzuri ambayo imejengwa kwa juhudi kubwa yetu sote hasa suala la kumaliza mashauri kwa wakati na kwa ubora. Hii ni muhimu katika Utawala Bora wenye kujali Demokrasia jambo ambalo Tanzania ni muasisi wake. Hivyo nawaasa kuzingatia Dira ya Mahakama ya “Upatikanaji wa Haki kwa Wakati na kwa Wote,” amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu suala la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA)  amesema  amejifunza kuwa yawainua pia katika ubora kazi zao. Na ni matokeo ya juhudi kubwa ya viongozi wa Mhimili huo,akiwemo Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe.  Mohamed Chande Othman na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahimu Hamis Juma, ambaye hana mchezo pale mtumishi anaposhindwa kuendana na TEHAMA.

 

Ameiomba Mahakama ya Tanzania kuendelea na utaratibu wa mafunzo na semina za ndani na nje ya Tanzania mara kwa mara ili yawe endelevu kwa watumishi wote.

Mhe. Jaji Mzuna, ambaye ametumikia katika kipindi cha miaka 33 ya utumishi wake anaishukuru Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka nchini (DPP) na Mawakili wa Kujitegemea   ambao walimsaidia  kuhakikisha kwamba mashauri yanaisha kwa wakati. Walijitolea ujuzi na maarifa yao katika kusaidia Mahakama ili kufikia uamuzi wa haki. Pia anawashukuru watumishi wenzake wa kada zote, Mawakili wa Serikali, Mawakili Binafsi na Viongozi wa Dini ambao siku zote wanatuombea. Huku akisema.

“Hii ni siku ya furaha kwangu maana si wote waliweza kufikisha umri wa kustaafu. Zamani tuliagwa baada ya kifo. Nashukuru siku hizi unaagwa ukiwa hai,”.

Jaji Mstaafu huyo amesema ana ujumbe wa kuacha kama alivyotoa Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Barnabas Samatta aliwahi kusema katika hotuba yake aliyoitoa jijini Dar es Salaam tarehe 4 Mei, 2001.  Alimnukuu Lord Chancellor Lyndhust, Kiongozi Mkuu wa Majaji huko Uingereza alipoulizwa swali kuwa ungependa Majaji wako wawe na sifa gani? Naye alijibu kama ifuatavyo:-“Kwanza, lazima awe mwaminifu,Pili, ni lazima awe na juhudi katika kazi,Tatu awe na ujasiri na Nne, ni lazima awe muungwana. Halafu kama ana ujuzi fulani wa sheria itasaidia.”

Kwa upande wake Jaji Victoria amesema alistaafu rasmi  Utumishi wa Umma siku ya tarehe 04 Mei, 2023 ambayo pia ndio siku yake ya kumbukizi ya kuzaliwa.

Amesema kazi ya kuamua mashauri ni kazi nzito, kwa hiyo pamoja na kutumia sheria na kufuata kanuni za maadili zilizoanishwa, wanahitaji nguvu ya ziada na pia jicho la pili na hilo linapatikana kwa Mwenyenzi Mungu. Hivyo katika hilo anashukuru kanisa linalonipa huduma ya kiroho. Katika kipindi chote cha utendaji wake wa kazi ndani Mahakama, kwani  kuna mambo aliyojifunza:

“Nimejifunza kujituma na kujitolea. Watumishi wa Mahakama katika kada zote wanajituma sana. Kwa mfano Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili na Mahakimu hawana muda maalum wa kazi kwani muda wote wako kazini. Wasipokuwa mahakamani basi ujue wamebeba majadala kufanyia kazi nyumbani. Hii inaonyesha jinsi ambavyo wako ‘committed’ katika kutoa huduma kwa wadaawa ili kutimiza dhima ya Mahakama ya Utoaji Haki kwa Wakati kwa Wote,” amesema Mhe. Jaji Victoria.

Ameyataja mambo mengine aliyojifunza ni kwamba mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo katika Mhimili. Hapa kuna mahusiano ya kitaaluma (collegiality) na yale ya kijamii (social cooperation). Hivyo kikazi, Majaji na Mahakimu wanasaidiana  kwa kuelekezana, kwa majadiliano na hata kubadilishana nyaraka.

Mhe. Jaji Victoria amesema kwa upande wa mahusiano ya kijamii yako vizuri watumishi wa Mahakama wamekuwa mstari wa mbele kusaidiana katika shughuli za kijamii hasa misiba, ugonjwa na harusi. Huku akisema yeye ni shahidi wa mahusiano hayo  kwani mwaka 2019, 2020 na 2021 aliwapoteza kaka zake watatu na mama mkwe. Katika misiba yote hiyo alipata faraja.

Jambo jingine   amejifunza kuwa Mahakama ni Mhimili mkubwa kikazi na hata Kimamlaka. Mahakama ipo Tanzania nzima. Ziko Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mkoa. Na Mahakama Kuu zaidi ya Kanda 20 na Divishen tano. Idadi hii inaonyesha kuwa          Mahakama ni Mhimili ambao Mamlaka yake imeenea mpaka katika ngazi ya chini.

Akitolea mfano kwamba Mahakama za Mwanzo zinatoa huduma mpaka katika vijiji. Wengi wetu tumezoea kuona Mahakama za Wilaya/Mkoa, Mahakama Kuu na Rufani lakini wakumbuke kuwa Mamlaka ya Mahakama ipo na inawafikia wananchi katika ngazi ya chini kabisa ya Mahakama za Mwanzo.

“Kuna sehemu ambazo mazingira yake magumu, lakini Mahakama imekuwa ikijua umuhimu wa huduma yake kwa hiyo inapeleka Mahakimu ambao wanahudumu na kuondoka (Visiting Magistrates). Mfano ni Mahakama ya Mwanzo Masela iliyopo kwenye Kijiji wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.

Mhe. Jaji Victoria aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 25 Julai, 2015. Hapo ndipo safari yake katika Mhimili huu ilipoanzia baada ya kuwa Wakili wa Kujitegemea kwa zaidi ya miaka 20. Kabla ya uteuzi  huo , alitokea katika ofisi ya uwakili ya VELMA Law. Toka uteuzi mwaka 2015 amehudumu katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga na baadaye Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi. Nimefanya pia sessions Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Divisheni ya Biashara.

Majaji wote alama kuu tunazoacha ni maamuzi yetu. Nina furaha kuwa nimeacha judgments na rulings zakutosha. Nyingi zipo Tanzilii na nyingine zipo tu kwenye majalada. Ni matumaini yangu kuwa zitasaidia kwa njia moja au nyingine katika maendeleo ya sheria. Pia nafurahi kusema kuwa nimestaafu bila kuwa na pending judgments au rulings za kuandika. Kwa hivyo nitahesabika kati ya wale majaji ambao tumeondoka bila kudaiwa maamuzi yeyote.

Kuhusu wasifu wa Mhe.Jaji Mzuna alizaliwa tarehe 15 Julai, 1963 katika Kijiji cha Kumsenga, Tarafa ya Mabamba, Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto sita. Alianza Shule ya Msingi Kumsenga, Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma mnamo Januari, 1972 hadi Oktoba, 1978. alikuwa mmoja wa waanzilishi wa shule hiyo. ana faraja pia kusema kuwa alikalia dawati kwa mara ya kwanza siku anafanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba baada ya kuyaazima shule jirani ya Nyarugunga, yapata kilometa nne,waliyabeba kichwani.

Alipata Elimu ya Sekondari 1979 -1982 alipohitimu kidato cha nne pale Sekondari ya Mpwapwa, Dodoma. Aidha, 1983 -1985 alijiunga na Sekondari Songea Boys’ mkoani Ruvuma kwa masomo ya kidato cha tano na sita. Mwaka1985-1986 nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupora na hatimaye kumalizia Mugulani, Dar es Salaam. Mnamo Julai, 1986 -1989 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na hatimaye kutunukiwa Shahada ya Sheria (LL.B  with Hons). Baadae Alijiunga na mafunzo kazini yaani “Internship” Dodoma na Dar es Salaam.

Kuhusu ajira, niliajiriwa kama Hakimu Mkazi, tarehe 31 Machi, 1990. Alihudumu kwa nafasi hiyo Mkoa wa Mwanza kabla ya kuteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya za Mwanza (1997), Lushoto (1998-2000) Baadae Hakimu Mkazi Mfawidhi Mikoa ya Mbeya (2000-2001), Singida (2001- 2003), Bukoba/Kagera (2003-2005), Dodoma (2005-2007).

 

Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa. Mnamo tarehe 26 Juni, 2009, aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,kituo chake cha kazi kikiwa Moshi, Kilimanjaro. Mnano 2003-2005 aliteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara.

Wadhifa huo aliendelea nao mwaka 2005 mpaka 2006 Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mwaka 2006 hadi 2008 alihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Dar es Salaam. Mnamo  mwaka 2008-2022 alihamishiwa Arusha kwa nafasi hiyo hiyo ya Jaji Mfawidhi. Kituo chake cha mwisho katika utumishi huo ni Masjala Kuu Dar es Salaam, akiwa Jaji Mfawidhi, Kazi Maalumu 2022 hadi Julai 2023.

Lakini kabla ya hapo alishiriki mafunzo mbalimbali ya kujengeana uzoefu kazini ndani na nje ya nchi katika utumishi wake pia, alitekeleza majukumu mengine mfano Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Mwanza na Mbeya.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Moses Mzuna.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Mhe. Victoria Makani(kushoto) akiwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo(kulia) ambaye alifanya naye kazi. 


Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani katika hafla hiyo.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Moses Mzuna(kushoto) akiwa na mkewe(kulia) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki(katikati).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani(katikati w) akiwa katika picha ya pamoja, Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Moses Mzuna(wa pili kushoto) na Mhe. Victoria Makani(wa pili kulia), ambao wamestaafu katika utumishi wa umma.Waliosimama ni familia ya Mhe. Jaji Victoria. Picha za chini ni Viongozi wa Mahakama ya Tanzania, na baadhi ya   familia za Majaji hao waliostaafu.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni