Ijumaa, 1 Septemba 2023

JUKWAA MAJAJI WAKUU MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA KUFANYIKA TANZANIA

Na Faustine Kapama-Mahakama

Mahakama ya Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika utakaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 23 hadi 27 Oktoba, 2023.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 1 Septemba, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Mhe, Ignas Kitusi alipokuwa anaongea na Wahariri na Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.

“Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (SEACJF) utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” Mhe Kitusi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania amesema.

Amesema Mkutano huo utahudhuriwa na Majaji Wakuu 16 kutoka Angola, Botswana, Eswatin, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania Bara, Tanzania Visiwani (Zanzibar), Uganda, Zambia na Zimbamwe.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa Jukwaa hilo ni sehemu muhimu ya kukuza ushirikiano, kubadilishana maarifa na maendeleo ya mifumo ya Mahakama ndani ya eneo la Kusini mwa Afrika.

“Jukwaa hili pia ni sehemu ya kujadiliana juu ya changamoto zinazowakabili katika mfumo wa utoaji haki na kubadilishana mbinu bora na kushughulikia changamoto zinazokabili Mahakama katika Nchi zetu,” amesema.

Mhe. Kitusi amesema kuwa Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Wajibu wa Mahakama za Kitaifa katika Utatuzi wa Migogoro kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AFCFTA): Matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Amesema kuwa kulingana na kaulimbiu hiyo kusisitiza biashara huria, wakati Mkutano huo kutakuwepo na matukio muhimu ambayo yatakuwa yakiendelea, ikiwemo mijadala na mawasilisho kutoka kwa wanasheria na wanazuoni kutoka maeneo mbalimbali ya Nchi za SADC.

“Kutakuwepo pia na maonesho ya wadau mbalimbali wa Mahakama yatakayokuwa yakiendelea katika Viwanja vya Hoteli ya Mount Meru kuanzia tarehe ya ufunguzi tarehe 23 Oktoba hadi ufungaji wa Mkutano tarehe 27 Oktoba, 2023,” amesema.

Wadau hao wanaotegemewa ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Biashara, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Kutakuwepo pia na Bodi ya Utalii (TTB), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mabenki, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), Shirika la Maendeleo la Taifa (TPDC) na wengine.

“Lengo la kuwaalika wadau hawa ni kuwaonyesha wageni wetu huduma mbalimbali zinazotolewa nchini na kuungana na Serikali kutangaza vivutio nchini ikiwemo kuunga mkono Filamu ya ‘Royal Tour,” Mhe. Kitusi amesema.

Amesema kuwa jukwaa hilo la Majaji Wakuu limekuwa likikutana kila mwaka katika moja ya Nchi mwanachama kwa lengo la kuelimishana na kubadilishana uzoefu wa utatuzi wa changamoto mbalimbali ili kuboresha huduma ya utoaji wa haki kwa wananchi.

Mkutano huo wa Wahariri na Waandishi wa habari umehudhuriwa pia na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Martha Mpaze, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Elimu na Habari, Bw. Machumu Essaba na sehemu ya wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Mkutano huo.

Katika kutambua na kukuza jukumu muhimu la Mahakama ndani ya Kanda, Majaji Wakuu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika waliamua kuanzisha Jukwaa mwaka 2003 ili, pamoja na mambo mengine, kuzingatia Utawala wa Sheria, Demokrasia, Uhuru wa Mahakama na kukuza mawasiliano ya pamoja.

Maono au mtazamo wa Jukwaa hilo ni kuwa na Mahakama iliyobadilika, iliyo huru, iliyounganishwa na yenye umoja ambayo inakuza utawala wa sheria, haki, demokrasia na utawala bora ili kuhakikisha ustawi, usawa, amani na usalama wa raia wote.

Kanuni zinazoongoza utendaji kazi na uendeshaji wa umoja huo ni kukuza utawala wa sheria, utoaji wa haki bora inayopatikana kwa wote, utawala bora na maadili ya pamoja, uwazi, uhuru, kutopendelea, uadilifu na uwajibikaji, kukuza utamaduni wa haki za binadamu, uhuru, uvumilivu na kuishi pamoja kwa amani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Mhe, Ignas Kitusi akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali leo tarehe 1 Septemba, 2023. Picha chini, Mhe. Kitusi akiwaonyesha moja ya nyaraka muhimu zitakazotumika katika Mkutano huo.

 Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akifuatilia kwa karibu kilichokuwa kinaendelea kwenye Mkutano huo.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Elimu na Habari, Bw. Machumu Essaba akitoa maelezo ya utangulizi katika Mkutano huo.
Meza Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Mhe, Ignas Kitusi (katikati), Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Elimu na Habari, Bw. Machumu Essaba (kulia).
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile akiwasilisha neno la shukrani kwa Mahakama ya Tanzania kuandaa mkutano huo.
Sehemu ya Wahariri na Waandishi wa Habari (juu na chini) waliohudhuria mkutano huo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni