Ijumaa, 1 Septemba 2023

WADAU MOROGORO WAVUTIWA NA NAMNA MIFUMO YA MAHAKAMA INAVYOFANYA KAZI

Na. EVELINA ODEMBA – MAHAKAMA MOROGORO.

Wadau wa Mahakama Mkoa wa Morogoro waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kupata huduma waonesha shauku yao ya kuvutiwa na namna Mahakama iliyojidhatiti na kuboresha mifumo yake ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yake ya kusajili mashauri na kuyaendesha.

Mifumo hiyo ya TEHAMA iliainishwa wakati wa utoaji wa elimu kwa umma, kupitia elimu hiyo wadau walipitishwa kwenye mfumo wa kusajili mashauri (JSDS 2) na kuelezewa namna unavyofanya kazi huku wakijulishwa kuwa sasa mteja anaweza kupata taarifa za kesi yake kwa usahihi kupitia mfumo huo ikiwemo kujua tarehe iliyopangwa kwa shauri lake kusikilizwa na kufahamu Jaji au Hakimu anayesikiliza bila kufika Mahakamani kuulizia taarifa hizo.

Elimu hiyo ilitolewa na wasaidizi wa kumbukumbu Bw. Shukuru Kilo anayeshugulika na usajili wa mashauri ya Madai na Bw. Boniphace Masubo anayesajili mashauri ya Jinai wakisaidiwa na Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogogoro Mhe. Augustina Mmbando ambaye alikuwa akifafanua masuala mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza na kuhitaji ufafanuzi zaidi. 

Wateja hao walitoa pongezi zao kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa maboresho hayo ya teknolojia inayowafikilia watanzania na wadau wa Mahakama kupata taarifa kupitia mawasiliano hayo hasa wakati wa kufungua mashauri au kuahirishwa kwa kesi hivyo wanaepuka gharama za kufika mahakamani.

Wadau hao walipata wasaa wa kuuliza maswali na miongoni mwa maswali hayo yaliyoulizwa ni kuhusu usalama wa taarifa za mashauri yao zinazowekwa kwenye mfumo zinavyoweza kuhifadhiwa bila kupotea.

Naibu Msajili Mhe. Augustina Mmbando alitolea ufafanuzi kuwa Mahakama ina Seva zidi ya mbili zenye ukubwa wa kutosha hivyo taarifa zinahifadhiwa kwenye Seva zaidi ya moja hivyo wasitie shaka kuhusu usalama wa taarifa zao huku akiwasisitiza kujaza taarifa zao sahihi ili kunapotokea mrejesho waweze kupatikana kwa haraka.

Aidha, wateja walipata wasaa wa kujionea namna mfumo wa usikilizaji mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao unavyofanya kazi na walielezewa kuwa kwa sasa unaweza kusikiliza kesi yako bila kufika mahakamani ulikofungulia shauri lako. Unachotakiwa kufanya ni kutoa taaarifa tuu.

Mahakama ya Tanzania imejikita katika matumizi makubwa ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo kupitia mifumo yake imekuwa ikitoa taarifa kwa mteja juu ya mwenendo wa kesi toka inapofunguliwa hadi inapomalizika kusikilizwa, pamoja na kusikiliza mashauri kwa njia ya mahakama mtandao “video conferencing” kumeokoa gharama kubwa kwani mdaawa anaweza kufatilia kesi yake wakati akiendelea na shughuli zake za kiuchumi.

Msaidizi wa kumbukumbu kutoka Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mjini Morogoro Bw. Shukuru Kilo akitoe elimu kwa wateja wa Mahakama (hawapo pichani) ya namna mifumo ya Mahakama inavyofanya kazi. 

Msaidizi wa Kumbukumbu Bw. Shukuru Kilo akiwaonesha wateja wa Mahakama namna ya kuingia kwenye mfumo wa kusajili mashauri wa JSDS 2 wakati akitoa elimu kwa wateja hao katika vipindi vya elimu vinavyoendelea kutolewa kupitia Kituo cha Utoaji Haki Morogoro.

Mteja wa Mahakama (aliyesimama) akiuliza swali la namna usalama wa taarifa za mteja kupitia mfumo.

Sehemu ya wateja wakifuatilia elimu kwa umakini

Mahakama mtandao iliyotumika kutolea elimu ambayo wateja walielekezwa kwa mfano namna mashauri yanavyoweza kusikilizwa kwa njia hiyo.

Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni