Ijumaa, 1 Septemba 2023

ASKARI ALIYESHITAKIWA KWA KUUA BILA KUKUSUDIA AACHIWA HURU

Na Evelina Odemba- Mahakama, Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, imemuachia huru bila masharti yeyote Askari wa Jeshi la Polisi mwenye Namba G.88808 Koplo Mapalala aliyekuwa anakabiliwa na shtaka la kuuwa bila kukusudia.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Messe Chaba hivi karibuni baada ya kusikiliza ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka na utetezi. Katika shauri hilo, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Elias Masini wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Msomi Fredy Sanga.

Koplo Mapalala alikabiliwa na shtaka la kumuua Hamis Mng’ombe (30), Mkazi wa Mvua, tarehe 31 Mei, 2022 katika mazingira yaliyopelekea kutumia risasi za moto ili kuwatawanya wananchi wenye hasira kali waliokuwa wamemzunguka.

Akisoma hukumu ya shauri hilo, Mhe. Chaba alizingatia shufaa zilizowasilishwa na upande wa utetezi kuwa mshitakiwa alikuwa kwenye kutekeleza majukumu yake ya kazi ambapo alijikuta amezingirwa na kundi la watu wenye silaha za jadi wakiwa na lengo la kumzuru.

Mhe. Chaba alieleza kuwa wakati akijitetea kulinda silaha na kuutetea uhai wake Askali huyo alifyatua risasi iliyompata marehemu kwenye mguu na kusababisha jeraha lililopelekea kifo chake baada ya kuvuja damu nyingi.

Hata hivyo, alitoa onyo kuwa kalamu ya Askali ni bunduki, hivyo wanapaswa kuitumia vizuri kuleta amani sehemu yenye uvunjifu wa amani na sio kuitumia kukatisha uhai.

Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili Sanga alisema kuwa wamepokea kwa furaha uamuzi huo na kuipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa iliyoyafanya kwakuwa imeweza kusikiliza kesi hiyo ndani ya mwaka mmoja.

“Tunafurahishwa na maboresho yanayofanywa na Mhimili wa Mahakama, kesi hii imechukua mwaka mmoja tu, jambo ambalo miaka mitatu nyuma lilikuwa ndoto,” alisema.

Alibainisha kuwa hapo awali walikuwa wanategemewa Majaji kutoka Dar es Salaam wapangiwe kikao maalumu ndipo waje kusikiliza, lakini kwa sasa tunashuhudia shauri limesikilizwa na Jaji wa hapa, kwa kweli Mahakama inafanya vizuri,” alieleza.

Kesi zingine 11 zitasikilizwa katika kikao hiki mbele ya Mhe. Chaba aliyeanza tarehe 28 Agosti,2023 na anategemea kuhitimisha tarehe 22 Septemba, 2023.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba.

Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni