Na Eva Leshange- Mahakama, Singida
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amewahimiza watumishi
wa Mahakama mkoani Singida kudumisha upendo, ushirikiano na mshikamano mahala
pa kazi.
Mhe. Dkt. Masabo alitoa
wito huo hivi karibuni alipokuwa anaongea na watumishi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi na Mahakama za Mwanzo kwenye ziara yake ya kikazi mkoani hapa. Alisema kuwa
mambo hayo matatu yakitekelezwa yatafanya mahala pa kazi kuwa pazuri na rafiki
kwakuwa watumishi hutumia muda mwingi wakiwa kazini.
“Watumishi wenzangu,
nasisitiza tuimarishe upendo, ushirikiano na mshikamano mahala pa kazi kwani
tunatumia muda mwingi kazini. Tushikamane, tubebeane mapungufu na tuinuane
tunapo anguka,” alisema.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwapongeza
Mahakimu na watumishi wa kada zingine kwa kazi nzuri wanayofanya, hasa katika
usikilizaji wa mashauri. Aliwataka kuongeza kasi zaidi na kuhakikisha hakuna mlundikano
wa mashauri.
Aliwakumbusha Mahakimu kufikia
kipimo kilichowekwa na Mahakama chz kumaliza mashauri, hivyo kila mmoja anatakiwa
kujitathmini kama amefikia malengo kwa kiasi gani.
Mhe. Dkt. Masabo aliwasisitiza
Mahakimu kuwa waadilifu, kwani kazi ya kutoa maamuzi ni kazi ya kimungu ambayo haiwezi
kufanyika pasipo uadilifu.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi
alisisitiza malipo ya mirathi kufanyika ipasavyo kwa wanufaika na kuhimiza jitahada
binafsi zifanyike kwa kufanya upekuzi kwenye majalada yote ambayo mirathi haijafungwa
ili kubaini kama kuna wanufaika ambao hawajalipwa.
Katika ziara yake mkoani
hapa, Mhe. Dkt. Masabo alipata fursa ya kutembelea Gereza la Wilaya Singida na
kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu.
Aliwapongeza wadau wote wa haki jinai kwa kazi
nzuri wanayofanya, kwani hali ya Gereza hilo inaonekana kuwa nzuri, hakuna
msongamano na changamoto zote zilizoibuliwa zilitolewa majibu.
Sehemu ya watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi na Watumishi wa Mahakama za Mwanzo mkoani Singida
wakisalimiana na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe
Dkt. Juliana Masabo alipokua kwenye ziara ya kikazi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Singida, Mhe. Allu Nzowa akimkaribisha Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyeketi mbele kulia) akiwa ameambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi (aliyeketi kushoto)
Sehemu ya watumishi
wakijitambulisha Mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt.
Juliana Masabo (aliyekaa mbele katikati). Anaye jitambulisha ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe. Ferdnand Njau.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akisalimiana na wajumbe wa haki jinai alipowasiri Gereza la Wilaya Singida kwa ajili ya ukaguzi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni