Ijumaa, 1 Septemba 2023

SIMULIZI YA KUSISIMUA YASHAWISHI WANAFUNZI KUPENDA KUWA MAHAKIMU

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha

Wanachama wa Club ya Mahakama katika Shule ya Sekondari Gili iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani wamefunguka kuuliza maswali mengi na kutaka kujua hatua muhimu za kuwafanya wawe wanasheria au Mahakimu.

Hamu ya kufikia hatua hiyo ilikuja baada ya wanafunzi hao kupata histori ya Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona aliyowaeleza alipokuwa anatoa elimu ya sheria katika club hiyo.

Akisimulia historia yake, Mhe. Kibona alisema wakati yuko kidato cha pili siku moja usiku akiwa anasoma kwa mtindo wa kuweka miguu kwenye beseni la maji ili asisinzie alisikia kishindo cha mtu anaruka uzio.

Anaeleza kuwa alipoinuka alikuta ni mwizi, akamkamata na kumpeleka polisi, baadaye aliitwa mahakamani kutoa ushahidi wa namna alivyomuona mwizi huyu.

Mhe. Kibona alisema baada tu ya kufika mahakamani alimuona Hakimu amevaa suti nyeusi ameketi katika kiti anaendesha kesi, alivutiwa namna anavyouliza maswali.

Alieleza kuvutiwa na kazi hiyo, hivyo akafuatilia namna gani anaweza kuwa Hakimu na mpaka leo ndoto yake imetimi na anajivunia kuwa miongoni wa watu wanaotoa haki katika jamii.

Baada ya simulizi hiyo, wanafunzi katika shule hiyo walijawa na shauku na kutaka kujua zaidi vigezo vunabvyotumika mpaka mtu kufikia kuwa mwanasheri au Hakimu.Wanafunzi hao walitaka pia kujua tofauti iliyopo kati ya Hakimu na mwanasheria.

Elimu katika Club ya Mahakama kwenye Shule ya Sekondari Gili hufanyika kila mwezi. Utoaji wa elimu hii ya kisheria ilizindiliwa mwezi wa saba mwaka huu.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona (juu) akisimulia historia yake kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Gili. Picha pichi wanafunzi hao wakimsikiliza.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni