Na Hilari Herman-Mahakama, Lindi
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim hivi karibuni aliongoza kikao maalumu
alichokiitisha kujadili namna watakavyofanikisha kuunda kamati za utoaji elimu
katika ngazi zote za Mahakama katika Kanda hiyo.
Kikao
hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Mtwara na kuhudhuriwa na wadau wa
haki jinai na Viongozi wa Kanda hiyo, huku Mahakimu wengine wakishiriki kwa
njia ya Mtandao (video Conference).
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhe. Ebrahim alisema hiyo ni ishara ya uzinduzi wa kamati za
utoaji elimu kwa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi na Mahakama zote
za Wilaya na Mwanzo zilizopo katika Kanda hiyo ili kurahisisha zoezi la utoaji elimu
kwa wananchi kwa kugusa nyanja zote.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa moja ya malengo ya
Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni kurudisha imani ya wananchi kwa
Mahakama, hivyo alisisitiza jukumu hilo haliwezi kufanywa na Mahakama pekee,
bali kwa kushirikiana na wadau wote wa haki katika majukwaa mbalimbali ya
utoaji elimu.
“Najua
kila taasisi ina namna ya kuwafikia wananchi, lakini uongozi wa Mahakama Kanda
ya Mtwara umeona kuwashirikisha ninyi wadau kwani tunaowajibu wa kuwafikia
wananchi kwa umoja wetu ili kuweza kushughulikia matatizo na kero zao tukiwa
kama timu moja yenye kutaka kusongeza mbele gurudumu la utoaji haki kwa wakati,”
alisema Mhe. Ebrahim.
Wadau
walifurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania na kuahidi
kutoa ushirikiano katika zoezi zima la utoaji elimu kwa jamii ili kupunguza
kero na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Wadau, Mahakimu na Viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (aliyekaa katikati), kushoto kwake ni Naibu Msajili, Mhe. Fredrick Lukuna na Kulia kwakwe ni Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Mtwara, Bw. Richard Mbambe.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni