Na Hasani haufi – Mahakama, Songea.
Jopo
la Majaji wa Mahakama ya Rufani, likiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma, limekamilisha kusikiliza mashauri 33 kati ya 34
yaliyokuwa yamepangwa kwenye kikao kilichokuwa kinafanyika katika Masjala ndogo
ya Mahakama hiyo Songea, Mkoa wa Ruvuma.
Majaji
hao wamekamilisha kusikiliza mashauri hayo ya rufaa yanayohusu ubakaji, mauaji.
matumizi mabaya ya madaraka na mengine kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 14
Agosti, 2023 hadi tarehe 25 Agosti, 2023, badala ya wiki tatu zilizokuwa
zimeratibiwa hapo awali.
Kasi
hiyo imeshangaza na kuibua hisia kubwa kutoka kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na
kuamini kwamba jitihada za kuboresha majengo ya Mahakama kweli zinaendana na
huduma bora na utoaji wa haki kwa wakati kwa wananchi.
Uchapakazi
na weledi mkubwa wa Majaji hao wa Mahakama ya Rufani pia umechochea kumaliza kwa
muda mfupi rundo la mashauri hayo ambayo yanahitaji umakini mkubwa wakati wa
kuyasikiliza.
Aidha,
ushirikiano wa watumishi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania pamoja na Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea umechagiza kwa kiasi kikubwa kufanikisha zoezi
hilo, ukiachilia mbali ugeni wa kikao hicho Songea.
Majaji
wengine walioungana na Jaji Mkuu kusikiliza mashauri hayo ni Mhe. Dkt. Gerald Ndika,
Mhe. Rehema Kerefu na Mhe. Sam Rumanyika. Katika kikao hicho ni shauri moja tu
ambalo liliahirishwa hadi kikao kijacho kutokana na sababu kadhaa.
Tarehe 14 Agosti, 2023, Jaji Mkuu wa Tanzania alizindua kikao
cha kwanza cha Mahakama ya Rufani na kufungua Masjala ndogo ya Mahakama hiyo Songea,
hatua ambayo inatanua wigo wa upatikanaji wa haki karibu na wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Prof. Juma alisema
tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Mahakama 2020/2021-2024/2025 katika kusogeza huduma ya utoaji
haki karibu zaidi na wananchi.
Aliwaeleza wananchi waliofurika kushuhudia tukio hilo kuwa Mahakama
ya Tanzania imejipanga kuikabili changamoto ya
umbali unaowalazimu wananchi kutumia gharama na muda mwingi kufuata
huduma ya haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni